Sunday, 17 July 2016
Thursday, 23 June 2016
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki waadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma
Watumishi wakimsikiliza Katibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz P Mlima (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma |
Watumishi wakimsikiliza Katibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz P Mlima (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma |
Waliosimama ni Watumishi wapya waliojiunga na Wizara hivi karibuni wakitambulishwa wakati wa Mkutano wa maadhimisho ya Wiki ya utumishi wa umma |
Monday, 20 June 2016
MHE. WAZIRI BALOZI DKT. MAHIGA AKUTANA NA RAIS WA SERIKALI YA ZANZIBAR MHE. DKT. SHEIN
Rais wa Serikali ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dkt. Ali Mohamed Shein (kulia) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) aliotembelea Ikulu |
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (kulia) akizungumza
na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi
Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. |
Friday, 17 June 2016
Uhuru wa kufanya biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANI
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Uhuru wa kufanya biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda
kuwajulisha wafanyabiashara wa Tanzania na wananchi wote kwa ujumla
kuwa wanaweza kutumia fursa za biashara zinazopatikana katika soko la
nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuuza bidhaa zao
ndani ya nchi wanachama yaani Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda pamoja na
sisi wenyewe Tanzania .
Wafanyabiashara wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa ni haki yao
na ni utekelezaji wa malengo ya Jumuiya ambayo yemebainishwa katika
Mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kifungu namba 5
ambapo Jumuiya ilianzisha Itifaki ya Umoja wa Forodha (The East African
Community Customs Union).
Chini ya Itifaki hiyo wafanyabiashara wa Nchi Wanachama wana uhuru wa
kufanyabiashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki bila kutozwa ushuru
wa forodha ilimradi bidhaa zao zimezingatia vigezo na kufuata utaratibu
ulioainishwa katika Itifaki hii.
Japokuwa Sudan Kusini imeridhia kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki
bado fursa za kufanya biashara nchini humo hazijakamilika. Hii ni
kwasababu nchi hiyo imejiunga na Jumuiya hivi karibuni na hadi hapo
itakaporejesha ‘Instrument’ yaani zile hati za kujiunga na Jumuiya baada
ya kufuata utaratibu wa nchi hiyo, ndipo itakuwa mwanachama kamili
ambaye atafurahia matunda haya tunayoyaongelea hapa. Yaani, Sudani
Kusini itaingia kwenye utaratibu wa utekelezaji wa Itifaki na
makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa katika Jumuiya.
Ili mfanyabiashara hasa mdogo aweze kufanya biashara katika Soko la Jumuiya hii anapaswa kufuata utaratibu ufuatao:
a. Mfanyabiashara/ Msafirishaji anatakiwa kufika kwenye kituo
chochote cha forodha kilichopo mpakani akiwa na bidhaa yake anayotaka
kuuza kwenye Soko la Jumuiya.
b. Akiwa Kituoni hapo, msafirishaji atatakiwa kupatiwa cheti cha
Uasilia wa Bidhaa Kilichorahisishwa (Simplified Certificate of Origin)
ambacho hutolewa bure na ofisi za Mamlaka ya Forodha Tanzania zilizopo
mipakani.
c. Mfanyabiashara atatakiwa kujaza taarifa zinazotakiwa kwenye
cheti hicho kama vile jina kamili la msafirishaji, anuani, nchi
anayotoka, maelezo ya bidhaa na thamani ya bidhaa. Afisa forodha wa
kituo husika atajaza maeneo yanayomhusu na kugonga muhuri katika cheti
hicho.
d. Mfanyabiashara atatakiwa kuonesha cheti cha uasilia wa bidhaa
wakati akiingia kwenye nchi mwanachama anapotaka kuuza bidhaa hiyo.
e. Cheti cha uasilia wa bidhaa ni kwa ajili ya mfanyabiashara mdogo
mwenye bidhaa isiyozidi dola za Kimarekani 2000. Aidha, mfanyabiashara
mdogo halazimiki kuwa na wakala wa Forodha.
f. Mfanyabiashara mdogo anatakiwa kufuata taratibu zinazohitajika
na taasisi nyingine zinazohusika katika kuruhusu uingizaji / uagizaji wa
bidhaa kama vile:
· Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA),
· Shirikia la Viwango Tanzania (TBS) na mamlaka nyingine.
Wizara inatoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla iwapo
watakutana na vikwazo visivyo vya kiforodha wakiwa katika Nchi
Wanachama, wawasilane na Wizara kupitia Mawasiliano yaliyoanishwa hapo
juu.
Aidha, wafanyabiashara pia wanaweza kutoa taarifa za vikwazo
wanavyokutana navyo kupitia mfumo wa ujumbe mfupi kwa kuandika neno
‘NTB’ na kutuma kwenda namba 15539. Vilevile kwa madereva wa magari
makubwa wanaosafirisha mizigo kwenda Nchi Wanachama utaratibu umewekwa
ambapo madereva hao wanaweza kutoa taarifa za moja kwa moja kwa Jeshi la
Polisi kupitia namba 0713631780 iwapo watakutana na vikwazo visivyo vya
Kiforodha vya barabarani. Kadhalika wafanyabiashara pia wanaweza
kuwasilisha malalamiko yao juu ya Vikwazo visivyo vya Kiforodha kupitia
tovuti ambayo ni www.tradebarriers.org
Wizara inahimiza wafanyabiashara kutumia njia halali za kuvusha bidhaa
kwenye mipaka ya Nchi wanachama kwani njia zisizo halali (Njia za panya)
hupelekea wafanyabiashara wengi kudhulumiwa bidhaa au mali zao,
kuvamiwa, kuumia na wakati mwingine kuuza bidhaa kwa bei ya hasara.
Watanzania wanaweza kufanya biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki na bidhaa zao kutolipa ushuru wa forodha ilimradi wamezingatia
taratibu zilizokubalika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha,
mfanyabiashara atatakiwa kuwa na hati ya kusafiria pindi anapotaka
kuvuka mpaka kwenda Nchi Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 16 Juni 2016.
Wednesday, 15 June 2016
Katibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz P. Mlima ( wa nne kutoka kulia waliokaa)
akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki Balozi Liberat Mfumukeko anayefuata kushoto kwake, Makatibu
Wakuu kutoka Wizara zinazosimamia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
pamoja na wataalam kutoka Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
katika kikao cha Retreaty ya Makatibu Wakuu unaoendelea Mjini Moshi.
Tuesday, 14 June 2016
KATIBU MKUU AKIWA KWENYE SHEREHE ZA KUFUNGA MAFUNZO MAALUM YA JKT
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo maalum ya JKT akitoa salaam maalum ya kijeshi kwa Kattibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz P. Mlima |
Katibu Mkuu Balozi Dkt Aziz P. Mlima akimpongeza mmoja wa wahitimu waliofanya vizuri zaidi wakati wa mafunzo maalum ya JKT |
Katibu Mkuu Balozi Dkt Aziz P. Mlima akikagua gwaride liliondaliwa wakati wa sherehe za kufunga mafunzo maalum ya JKT |
Katibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz P. Mlima (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Jeshi mara baada ya kuwasili viunga vya Kikosi namba 832 KJ Ruvu tayari kwa ufunguzi wa sherehe za kufunga mafunzo maalum ya JKT wapili kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasrimali watu Bibi Mary Fidelis |
Katibu Mkuu Balozi Dkt Azizi P. Mlima (kushoto) akitembelea mradi wa shamba la migomba la Kikosi namba 832 KJ Ruvu kabla ya kuanza kwa sherehe za kufunga mafunzo maaalum ya JKT, wakawanza kulia Mkuu wa Kikosi hicho Luteni Kanali Charles Mbuge. |
Katibu Mkuu Balozi Dkt Aziz P. Mlima (wakwanza kushoto) akipewa maelezo na Mkuu wa Kikosi namba 832 KJ Ruvu Luteni Kanali Charles Mbuge (wapili kulia) alipotembelea mradi wa kufuga kuku unaosimamiwa na kikosi kabla ya kuanza kwa sherehe za kufunga mafunzo maalum ya JKT (operasheni kikwete) yalifanyika katika viwanja vya JKT Ruvu. Mafunzo haya ya wiki sita (6) yalihusisha watumishi 30 wa Wizara ( 13 kati yao wakiwa ni wasichana na 17 ni Wavulana) |
KATIBU MKUU AKUTANA NA BALOZI WA SWEDEN NCHINI
Katibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz P.Mlima na Mhe. Balozi Katarina Rangnit wakijadili jambo kwenye Mkutano uliofanyika Juni 13, 2016, Wizarani, wanaofuatilia kulia ni Wakurugenzi kutoka Wizarani Bw. Geoffrey Mwambe, Bw. Oswald Kyamani na Bw. Eliabi Chodota. |
Katibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz P Mlima
akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Sweden Nchini Mhe. Balozi Katarina
Rangnitt alipomtembelea Wizarani, Juni 13, 2016.
Katibu Mkuu
Balozi Dkt. Aziz Mlima na Mhe. Balozi Katarina Rangnitt wakiwasilikiza
Mkurugenzi Mkazi wa TMEA Dkt. Josaphat Kweka ( wa kwanza kushoto kwa
Balozi), Bi Sara Spant kutoka Ubalozi wa Sweden na Bw. Ulf Ekdahl
kutoka Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA) katika Mkutano uliofanyika
Wizarani Juni 13,2016 |
Thursday, 2 June 2016
HOTUBA YA MHESHIMIWA BALOZI DKT. AUGUSTINE PHILIP MAHIGA (MB), WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI AKIWASILISHA MAKADIRIO YA BAJETI YA MAPATO NAMATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017
HOTUBA YA MHESHIMIWA BALOZI DKT. AUGUSTINE PHILIP MAHIGA (MB), WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI AKIWASILISHA MAKADIRIO YA BAJETI YA MAPATO NAMATUMIZI YA WIZARA KWA
MWAKA WA FEDHA 2016/2017
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kutokana na Taarifailiyowasilishwa leo Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati yaKudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalamanaomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitishaMakadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote nakushukuru
kwa fursa hii adhimu ya kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu kwa mara
ya kwanza Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki. Aidha, naombanitumie nafasi hii adhimu kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya
Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia Uchaguzi Mkuu
uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015.
3. Mheshimiwa Spika, naungana
na walionitangulia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake
madhubuti na makini unaoakisi kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’. Sisi
sote ni mashahidi wa namna uongozi wake ulivyogusa si tu wananchi wa
Tanzania bali pia ulivyopokelewa na kuwa mfano wa kuigwa katika nchi za
bara la Afrika na duniani kwa ujumla. Sifa zake zinasikika kila pembe ya
dunia na kutufanya tutembee kifua mbele. Nampongeza sana kwa kumteua
Mheshimiwa Samia Suluhu kuwa Mgombea Mwenza na baadae kuchaguliwa kuwa
Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke katika historia ya nchi yetu.
Kuchaguliwa kwake kumeidhihirishia dunia hatua kubwa ambayo nchi yetu
imepiga katika kumpa fursa sawa mwanamke.
4. Mheshimiwa Spika, nichukue
nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa
kuchaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kipindi cha
pili katika uchaguzi ulioendeshwa kwa amani na usalama. Kadhalika,
nampongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), kwa kuteuliwa kuwa
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wizara yangu imefaidika
sana na uongozi wao na miongozo mbalimbali wanayoitoa katika utekelezaji
wa majukumu yetu.
5. Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu walionitangulia kuwashukuru na kuwapongeza watoa hoja waliozungumza kabla yangu wakiongozwa na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu waJamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango (Mb),Waziri wa Fedha
na Mipango ambao hotuba zao zimeweka msingi mzuri kwa kuainisha dira na
masuala muhimu ya kitaifa na kimataifa ambayo baadhi yake yanaangukia
katika majukumu ya Wizara yangu. Kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais
kujenga ‘Tanzania ya Viwanda’ na kama ilivyotafsiriwa katika Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021, Wizara yangu nayo imejielekeza katika kutekeleza ‘Azma ya Serikali ya kujenga Uchumi wa Viwanda’.
6. Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, Wizara
hii ni mpya baada ya kuunganishwa kwa zilizokuwa Wizara mbili za Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki. Kwa ajili hiyo, namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli kwa kuniteua kuwa Mbunge na Waziri wa kwanza wa Wizara
hii. Napenda kumuahidi mbele ya Bunge lako Tukufu kuwa nitatumia ujuzi
na uzoefu mkubwa niliouvuna katika nyanja za diplomasia ya kikanda na
kimataifa kuendelea kuipaisha diplomasia ya Tanzania.
7. Mheshimiwa Spika, kazi yangu
imefanywa kuwa nyepesi zaidi kutokana na ushirikiano mzuri na ushauri
tunaoupata mara kwa mara kutoka kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya uongozi wa Mheshimiwa Balozi Adadi Mohammed Rajab(Mb), na Makamu wake Mheshimiwa Kanali Mstaafu Masoud Ali Khamis (Mb) pamoja na Wajumbe wote wa Kamati hiyo. Wamekuwa wa msaada mkubwa sana kwa Wizara yangu katika utekelezaji wa majukumu.
8. Mheshimiwa Spika, ukiniona nasimama mbele
ya Bunge lako Tukufu kwa kujiamini ni kwa sababu ninao nyuma yangu
viongozi wenzangu, watendaji na wafanyakazi wanaonisaidia kutekeleza
majukumu yangu kwa ufanisi mkubwa. Napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt.
Susan Alphonce Kolimba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Aziz Ponary Mlima, Katibu Mkuu,
Mheshimiwa Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu,
Wakurugenzi, Mabalozi, Maafisa na Wafanyakazi walioko Makao Makuu,
Balozini na Ofisi ya Zanzibar kwa msaada mkubwa wanaonipatia. Uzalendo
wao, ari yao na imani yao kwangu, vinanipa kila sababu ya kuamini kuwa
malengo tuliyojiwekea katika Bajeti hii tutayatekeleza kwa ufanisi
mkubwa.
9. Mheshimiwa Spika, mwisho lakini si mwisho kwa umuhimu, namshukuru kwa dhati mke wangu mpendwa Mama Elizabeth Mahiga,Watoto na familia yangu yote kwa ujumla kwa
kunivumilia, kuniunga mkono na kunipa utulivu wa kutosha kuniwezesha
kuyakabili majukumu niliyopewa na Mheshimiwa Rais kutimiza matarajio ya
Watanzania.
10. Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa, naungana naWafanyakazi wa Wizara yangu kutoa salamu za pole na rambirambi kwafamilia za Watumishi wenzetu watatu, Marehemu Manfred Ngatunga, Marehemu Apolonia Mbogo Mwangosi na Marehemu Ezekiel Makonda, ambao walifikwa na mauti wakati wakiendelea kuitumikia Wizara na Taifa kwaujumla. Tuendelee kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani.Amina.
11. Mheshimiwa Spika, hotuba
hii imejumuisha shughuli zilizokuwa zikifanywa na iliyokuwa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na iliyokuwa Wizara ya
Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Hivyo, nitatoa taarifa ya mapato na
matumizi ya Wizara hizo kwa mwaka wa fedha 2015/2016 na kuwasilisha
Mpango na Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
TATHMINI YA HALI YA DUNIA
Hali ya Uchumi, Siasa na Usalama Duniani
12. Mheshimiwa Spika, hali
ya dunia imeendelea kuwa ya mchanganyiko wa matumaini na mashaka.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita dunia imepiga hatua kwenye
masuala kadhaa ya msingi kwa ustawi na mustakabali wa dunia. Katika
kipindi hiki tumeshuhudia kusainiwa kwa Mkataba wa Paris kuhusu
Tabianchi mwezi Desemba, 2015 ambao umesubiriwa kwa muda mrefu.
Kusainiwa kwa Mkataba huu kunatoa matumaini kwa nchi za Afrika na zile
zinazoendelea kwa kuwepo kwa uhakika katika Kudhibiti na Kukabili
athari na changamoto za tabianchi. Hii ni kutokana na ukweli kuwa nchi
zetu zinaathirika zaidi na athari za tabianchi wakati ni wachangiaji
wadogo sana wa tatizo hilo. Kusainiwa kwa Mkataba huu kunatoa fursa kwa
nchi maskini kufidiwa na kujengewa uwezo katika kukabiliana na
changamoto hizo. Hili ni jambo ambalo nchi yetu imekuwa mstari wa mbele
kulipigania na Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliongoza
jitihada hizi akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi wa Umoja wa
Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.
13. Mheshimiwa Spika, jambo
lingine la kutia matumaini ni kusainiwa kwa Malengo ya Maendeleo
Endelevu ambayo yanachukua nafasi ya Malengo ya Milenia ya mwaka 2000 -
2015 ambayo utekelezaji wake ulifikia tamati mwezi Septemba, 2015.
Majadiliano kati ya nchi zetu yaliyofikia malengo haya yalizingatia
uzoefu katika utekelezaji wa Malengo ya Milenia, haja ya kumalizia
viporo vya Malengo ya Milenia na umuhimu wa kuhakikisha kuwa malengo
mapya yanazingatia mahitaji ya leo na kesho kwa kuhakikisha kuwa ni
endelevu. Malengo ya Maendeleo Endelevu ndio mwongozo wa agenda ya
maendeleo duniani kote na ndiyo yatakayokuwa rejea ya majadiliano na
makubaliano mengine duniani. Sisi tumejipanga vyema kutekeleza malengo
hayo na bahati nzuri yanashabihiana kwa kiwango kikubwa na Dira yetu ya
Taifa ya 2025 na Mpango wa Pili wa Maendeleo 2016/2017 – 2020/2021.
14. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha mwaka mmoja uliopita kumekuwa pia na matukio ambayo yana
mwelekeo mzuri kwa ustawi wa amani na usalama duniani. Kwa kuwa yako
mengi, niruhusu niyataje mawili makubwa. Kwanza, ni hatua ya nchi za
Marekani na Cuba kuamua kurejesha urafiki wao baada ya kuwepo kwa
vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba kwa zaidi ya miaka 50. Hatua hii ni
muhimu na tunaungana na wapenda amani kote duniani kumpongeza Rais
Barack Obama wa Marekani na Rais Raul Castro wa Cuba. Ikumbukwe kuwa
Marekani na Cuba ni rafiki wa Tanzania, na Tanzania imekuwa mstari wa
mbele kupinga vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba. Ni faraja kuwa uhasama
huo umekwisha, kwani kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba
kutawezesha Cuba kushiriki kikamilifu katika uchumi wa Dunia, na hali
kadhalika itaimarisha ushirikiano mzuri wa kiuchumi tulionao kati yetu
na Cuba. Makubaliano hayo yamemaliza mabaki ya misuguano ya vita baridi
ya miongo ya nyuma na kuendeleza amani duniani.
15. Mheshimiwa Spika, tukio la pili, ni kuondolewa kwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Iran kuhusu Mpango wa Iran wa Nyuklia tarehe
16 Januari, 2016, kufuatia Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki
kuthibitisha kuwa Iran imekamilisha hatua zote ilizopewa na Wanachama wa
Kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Ujerumani. Hatua
hii nayo ni muhimu sana kwa kuwa inaondoa hali ya mashaka iliyokuwa
imetanda katika eneo la Mashariki ya Kati kuhusu nchi ya Iran
kutengeneza silaha za nyuklia. Mashaka
hayo ndiyo ambayo yamekuwa yakiyumbisha sana dunia kiuchumi kwa
kuathiri bei za mafuta. Iran ni nchi rafiki ambayo tunashirikiana nayo
kiuchumi. Hivyo, kuondolewa kwa vikwazo hivyo kunatoa fursa ya kukua kwa
ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili katika mazingira ya amani.
16. Mheshimiwa Spika, pamoja
na matumaini hayo, yako matukio na mambo ambayo yanaiweka dunia katika
hali ya tahadhari. Hali ya uchumi duniani haijaimarika sana na inapitia
katika mashaka makubwa. Hii inatokana na sababu kadhaa zikiwemo kupungua
kwa kasi ya ukuaji wa uchumi mkubwa wa China kutoka asilimia 6.9 hadi
asilimia 6.3; kushuka kwa bei ya bidhaa duniani kama dhahabu, mafuta,
shaba na bidhaa nyingine muhimu; na kupungua kwa mitaji na uwekezaji. Kuteremka
kwa bei ya mafuta hakujaleta unafuu sana kwetu kwa sababu bei ya bidhaa
zetu muhimu kwenye soko la dunia nazo zimeporomoka na thamani ya fedha
imepungua. Aidha, riba ya mikopo na mitaji imepanda. Hali
hii si afya kwa uchumi wa nchi masikini na zinazoendelea kwa kuwa
kushuka kwa bei ya bidhaa kunaathiri sana uchumi wa nchi zetu zenye
uwezo mdogo wa kuhimilimisukosuko ya uchumi wa dunia.
17. Mheshimiwa Spika, hali
ya usalama duniani nayo imeendelea kutoridhisha. Kumekuwepo na
kuongezeka kwa wasiwasi wa kiusalama kati ya Ulaya Magharibi na Urusi,
Korea Kaskazini na nchi za Asia hasa Korea Kusini inayosaidiwa na
Marekani, Syria na nchi za Mashariki ya Kati na kupanuka kwa shughuli na
dhana ya himaya ya Islamic State katika eneo lote la ukanda huo. Dhana hiyo inayosimamiwa katika eneo lote na kundi la Islamic State of Syria (ISS) imeanza kujipenyeza Afrika Mashariki, Magharibi na Kaskazini hasa Lybia. Dhana ya himaya hiyo au Caliphate ni
kali zaidi kuliko mlengo wa Al - Qaeda. Dunia inaelekea tena kwenye
ushindani mkali wa mataifa makubwa hasa kati ya Marekani, Urusi na
China. Kwa muktadha huo, Tanzania itaendelea kufuata siasa
isiyofungamana na upande wowote. Yote haya kwa pamoja yanaiweka dunia
katika hali ya tahadhari kubwa na hivyo kuilazimu dunia kuelekeza fedha
na muda wake mwingi katika ushindani na kutafuta ufumbuzi badala ya
kuelekeza muda na rasilimali hizo kujenga uchumi na kuinua hali ya
maisha ya watu. Tanzania imeendelea kutoa mchango wake wa moja kwa moja
na kwa kushirikiana na nchi nyingine katika kutatua migogoro ya Kanda na
kudumisha amani duniani. Kwa mantiki hiyo, Mheshimiwa Rais Mstaafu
Jakaya Mrisho Kikwete aliteuliwa kuwa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa
Afrika katika Mgogoro wa Libya na Mheshimiwa Rais Mstaafu Benjamin
William Mkapa aliteuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa Msuluhishi
wa Mgogoro wa Burundi. Uteuzi wa Viongozi wetu Wastaafu wa Kitaifa ni
ushahidi kuwa kauli ya Tanzania inasikilizwa na kuheshimika kwenye
majukwaa ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
18. Mheshimiwa Spika, Macho
na masikio ya dunia yameelekezwa huko Asia-Pacific kutokana na fukuto
la mgogoro wa umiliki wa eneo la Bahari ya Kusini mwa China unaohusisha
nchi za China, Brunei, Vietnam, Malaysia na Ufilipino. Pamoja na kuwa
kijiografia eneo hili laweza kuonekana ni mbali sana na nchi yetu,
athari za mgogoro huo zitagusa kila pembe ya dunia kama hautamalizika
kwa njia za amani. Eneo hilo ndio penye kitovu kikubwa cha ukuaji wa
uchumi, uzalishaji na biashara katika kipindi hiki ambacho uchumi wa
dunia kiujumla unasuasua. Tanzania inaamini kuwa njia ya uhakika ya
kumaliza mgogoro wa Bahari ya Kusini mwa China ni kupitia mazungumzo
baina ya nchi na nchi na kanda. Kwa sababu hiyo, tunaunga mkono juhudi
za utatuzi wa mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo na mashauriano.
Tunaitaka Jumuiya ya Kimataifa na vyombo vyake kuzingatia Azimio Na. 298
la mwaka 1982 la Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016
ILIYOKUWA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
19. Mheshimiwa Spika, kabla
ya kueleza utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa fedha
2015/2016, naomba uniruhusu niainishe kwa ufupi majukumu ya iliyokuwa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kama ifuatavyo:-
i. Kubuni na Kusimamia Utekelezaji wa Sera ya Nchi ya Mambo ya Nje;
ii. Kusimamia Mikataba na Makubaliano ya Kimataifa;
iii. Kuratibu Masuala ya Uhusiano baina ya Tanzania na nchi mbalimbali, Ushirikiano wa Kimataifa, Bara la Afrika na Kikanda;
iv. Kulinda na kuendeleza Maslahi ya Taifa ya Kiuchumi na Mengineyo nje ya nchi;
v. Kusimamia
masuala yanayohusu Kinga na Haki za Kibalozi kwa Wanadiplomasia waliopo
nchini kulingana na Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961;
vi. Kusimamia na kuratibu masuala ya Itifaki na Uwakilishi;
vii. Kuanzisha na Kusimamia Huduma za Kikonseli;
viii. Kuratibu shughuli za Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano; na
ix. Kusimamia utawala na Maendeleo ya Utumishi Wizarani na kwenye Balozi zetu.
20. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu hayo kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara ilitengewa kiasi cha
Shilingi 170,367,129,238.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi
162,367,129,238.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi
8,000,000,000.00 ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Katika fedha
zilizotengwa kwa Matumizi ya Kawaida, shilingi 153,698,142,238.00 ni kwa
ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi8,668,987,000.00 ni kwa ajili ya mishahara ya Watumishi.
21. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara na Balozi zake ilitarajia kukusanya maduhuli ya kiasi cha shilingi 20,036,019,000.00. Hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2016, Wizara imefanikiwa kukusanya kiasi cha
shilingi 16,296,907,020.00 ikiwa ni sawa na asilimia 81.3 ya makisio ya
makusanyo yote ya maduhuli kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
22. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2016 Wizara ilipokea jumla ya Shilingi 126,407,697,224.00 sawa na asilimia 77.8 ya bajeti iliyopitishwa na Bunge. Kati ya fedha hizo Shilingi 117,783,609,614.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi 8,624,087,610.00 ni kwa ajili ya mishahara ya Watumishi. Hadi hivi sasa, Wizara bado haijapokea mgao wowote wa fedha za bajeti ya maendeleo.
23. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara imetekeleza majukumu yake kama ifuatavyo:-
Kubuni na Kusimamia Utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje
24. Mheshimiwa Spika, Wizara
kwa kushirikiana na Balozi zake, Taasisi nyingine za Serikali na sekta
binafsi imeendelea kubuni na kusimamia utekelezaji wa Sera ya Mambo ya
Nje yenye lengo la kukuza uchumi wa nchi kupitia diplomasia ya uchumi
iliyo endelevu. Aidha, jukumu hili limepewa uzito zaidi na Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
wakati alipozindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ambapo aliziagiza Balozi zetu kushiriki Mikutano inayofanyika nje kwa
niaba ya Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Serikali. Jukumu hili
kubwa limetekelezwa ipasavyo na Balozi zetu na hivyo kupunguza gharama
kubwa za safari ambazo zingefanywa na Watumishi wa Wizara, Idara na
Taasisi za Serikali.
25. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kufanikisha ziara
za Viongozi Wakuu wa Kitaifa hapa nchini kutoka nchi za Vietnam na
Msumbiji. Wizara pia iliratibu ziara za viongozi mbalimbali kutoka nchi
za Saudi Arabia, Oman, Qatar, Ujerumani, Norway, Umoja wa Falme za
Kiarabu, Sweden, Finland, Ireland, Czech, Italia, na Urusi. Pamoja na
mambo mengine ziara hizo zililenga kuimarisha, mahusiano ya biashara na
uwekezaji kati ya nchi yetu na nchi hizo. Aidha,
baadhi ya nchi hizo tayari zina mikataba ya Ushirikiano na Tanzania na
nyingine zimeanzisha ushirikiano kwa mara ya kwanza.
26. Mheshimiwa Spika, Wizara
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilifanikisha kufanyika makongamano
na maonesho ya biashara na uwekezaji yaliyolenga kutangaza fursa za
biashara na uwekezaji zilizopo hapa nchini. Makongamano hayo
yalijumuisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania na nchi za Oman,
Urusi, Rwanda, Ujerumani, China, India, Czech, Comoro, Misri na
Singapore.
27. Mheshimiwa Spika, kutokana
na makongamano hayo, Tanzania iliweza kutangaza fursa zake mbalimbali
katika biashara na uwekezaji na kufanikisha yafuatayo:-
(a) Kusainiwa
kwa mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya Chama cha
Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Wakulima Tanzania na Chama cha
Wafanyabiashara wa Oman wa kuanzisha Kampuni ya Uwekezaji kati ya
Tanzania na Oman. Kampuni hiyo imeanzishwa kwa lengo la kutafuta fursa
za uwekezaji Tanzania na Oman na imeazimia kuanza na mtaji wa Dola za
Marekani milioni 25 ambazo zitatumika kutoa mikopo kwa wawekezaji.
Mkataba huo ulisainiwa mwezi Aprili 2016, Dar es Salaam wakati wa
Kongamano la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Oman;
(b) Serikali
ya Oman pia imeanza mazungumzo na kiwanda cha sukari Kagera kwa nia ya
kuingia makubaliano yatakayowezesha Serikali ya Oman kuwekeza katika
kiwanda hicho. Hatua hii inalenga kukiwezesha kiwanda kuzalisha tani
laki nne za sukari ambazo zitauzwa hapa nchini na hivyo kupunguza tatizo
la upungufu wa sukari. Ongezeko hili la uzalishaji pia litawezesha
kuzalisha hamira, spiriti na umeme. Hamira itauzwa Oman na sehemu
nyingine wakati umeme utaingizwa katika gridi ya taifa; na
(c) Kuanzishwa
kwa Kiwanda cha utengenezaji wa pikipiki katika eneo la Ukanda Maalum
wa Kiuchumi wa Bagamoyo kupitia Kampuni ya Guanghzhou Fekon Motorcycle
Co. Ltd. ya China. Aidha, Kampuni hiyo imeahidi kufungua Chuo maalum kwa
ajili ya mafunzo ya ufundi wa pikipiki na makenika. Vilevile, mwekezaji
huyo ameahidi kutoa nafasi kwa ajili ya vijana wa Tanzania kwenda China
kupata ujuzi wa masuala hayo katika kiwanda mama kilichopo China.
Makubaliano hayo yalifanyika wakati wa kongamano la biashara na
uwekezaji baina ya Afrika na China lililofanyika mwezi Agosti 2015 mjini
Guangzhou China.
28. Mheshimiwa Spika, Wizara
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika utekelezaji wa Sera ya
Mambo ya Nje imefanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali katika
sekta za miundombinu, nishati, viwanda, kilimo na mifugo. Baadhi ya
miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika mwaka wa fedha
2015/2016 ni pamoja na:-
(a) Mradi
wa barabara ya Ndundu-Somanga yenye urefu wa kilomita 60 uliozinduliwa
mwezi Agosti, 2015. Barabara hiyo imejengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa
Maendeleo wa Kuwait kwa kushirikiana na Mfuko wa Umoja wa Nchi
zinazozalisha Mafuta Duniani na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania;
(b) Mradi
wa ujenzi wa Barabara ya Kidahwe-Uvinza yenye urefu wa kilomita 76.6
uliozinduliwa mwezi Septemba, 2015. Barabara hiyo imejegwa kwa
ushirikiano wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia Mfuko wa
Maendeleo wa Abu Dhabi kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 57 pamoja
na mchango wa fedha za ndani;
(c) Mradi
wa Daraja la Kikwete kwenye mto Malagarasi mkoani Kigoma
lililozinduliwa mwezi Septemba, 2015. Daraja hilo limejengwa kwa
ushirikiano wa Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Korea
kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi wa Jamhuri ya Korea;
(d) Mradi
wa ujenzi wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha Tengeru, Arusha
kilichozinduliwa mwezi Agosti 2015 ambao ulitekelezwa kwa ushirikiano na
Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu; na
(e) Mradi
wa ujenzi wa bandari mpya ya Bagamoyo na Eneo Huru la Kiuchumi
uliozinduliwa Oktoba 2015. Mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano baina
ya Serikali ya Tanzania, China na Oman.
29. Mheshimiwa Spika, katika
hatua nyingine Wizara imeendelea kuzungumza na kuwashawishi wadau
mbalimbali wa maendeleo ili kusaidia jitihada za Serikali katika
kukabiliana na changamoto ya ujangili hapa nchini, hususan upatikanaji
wa vifaa kwa ajili ya kufanyia doria kwenye Mbuga na Hifadhi za Taifa. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba katika kipindi hiki, Serikali ya Ujerumani imeipatia Tanzania ndege mbili ndogo kwa
ajili ya kupambana na ujangili. Tunaamini kuwa ndege hizo zitaongeza
ari na ufanisi kwa askari wetu katika utekelezaji wa majukumu yao ya
kuendesha doria katika Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba yaliyopo
nchini. Vilevile, nchi nyingi za Ulaya, Marekani na Mashirika ya
Kimataifa kama vile World Wildlife Fund, Frankfurt Zoological Society zimeonyesha utayari wa kuisaidia Tanzania kwa hali na mali katika kulinda hifadhi za wanyamapori.
30. Mheshimiwa Spika, Kadhalika, Wizara kwa
kushirikiana na wadau wengine, imefanikisha majadiliano na Serikali ya
Ufaransa kwa ajili ya kusaidia mpango wa maboresho ya jengo la abiria (Terminal II) katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Serikali ya Ufaransa
kupitia Shirika lake la Maendeleo imekubali kuipatia Serikali ya
Tanzania kiasi chaEuro Milioni 65 kwa ajili ya ukarabati na uboreshaji wa uwanja huo.
31. Mheshimiwa Spika, Wizara
kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeendelea
kutafuta fursa za masomo nje ya nchi ili kuliwezesha Taifa kuwa na
hazina kubwa ya wataalam katika sekta mbalimbali. Napenda kuliarifu
Bunge lako Tukufu kuwa nchi rafiki za Algeria, Malaysia, Indonesia,
Pakistan, Iran, Malta, Misri, Sri Lanka, Brunei Darussalam, Canada,
Ujerumani, Uingereza, Marekani, Uholanzi, Ubelgiji, Oman, Urusi,
Australia, Japan, China, Cuba, Ufaransa, Thailand, Uswisi na Korea pia
zimeendelea kushirikiana nasi katika kuwajengea uwezo Watanzania kupitia
ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika fani mbalimbali.
32. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeratibu na kufanikisha upatikanaji wa mkopo wa masharti nafuu wa Dola
za Marekani milioni 20 kutoka Serikali ya Italia, kupitia Shirika la
Maendeleo la nchi hiyo. Mkopo huo utatumika kutekeleza mradi wa Technical and Labour Market Support Programmeunaolenga
kuimarisha na kukuza elimu ya Ufundi kwa kuvijengea uwezo vyuo vya
ufundi ili kutoa mafunzo yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira. Vyuo
vitakavyonufaika na mradi huo ni pamoja na Chuo cha Ufundi Dar es
Salaam, Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia
Mbeya.
33. Mheshimiwa Spika, Wizara
inaendelea na juhudi za kuwatafutia fursa za ajira na kuwaandalia
mazingira mazuri watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi.
Kufuatia Mkataba wa ajira baina ya Tanzania na Qatar, Watanzania wapatao
250 wamekwenda Qatar kufanya kazi kuanzia mwezi Desemba, 2015. Timu za
pande zote mbili zinaendelea na uratibu wa kuwapata Watanzania
watakaoweza kunufaika na fursa hiyo. Aidha, Wizara pia inaendelea
kuwasaidia Watanzania kupata kazi katika makampuni mbalimbali nje ya
nchi mathalani katika Mashirika ya Ndege yanayofanya safari zake hapa
nchini. Katika
mwaka wa fedha 2015/2016, Watanzania 18 walipata kazi katika Shirika la
Ndege la Emirates na jitihada kama hizo zinaendelea kufanyika kwa
mashirika mengine. Nichukue fursa hii kutoa wito kwa vijana wa Tanzania kujitokeza na kuomba kazi katika Mashirika ya Kimataifa.
34. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kufanikisha makubaliano kati ya Tanzania
na Poland yaliyofanyika mwezi Oktoba 2015, ambapo Poland ilikubali
kutoa mkopo wa masharti nafuu wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 110.
Makubaliano hayo yatawekwa saini baina ya Shirika la Maendeleo la Taifa
kwa upande wa Tanzania na kampuni ya URSUS ya Poland. Kati ya fedha
hizo, kiasi cha Dola za Marekani milioni 55 zitatumika kwa ajili ya
uanzishaji kiwanda cha kuunganisha matrekta hapa nchini yanayotengenezwa
na kampuni hiyo. Chini ya makubaliano hayo kampuni hiyo itafundisha
vijana wetu kuunganisha na kutengeneza matrekta. Aidha, kiasi cha Dola
za Marekani Milioni 55 kitatumika kwa ajili ya ujenzi wa maghala ya
kuhifadhia mazao. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa utekelezaji
wa miradi hii miwili utaanza hivi karibuni.
35. Mheshimiwa Spika,
katika suala zima la utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayoweka
msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi, Tanzania itaendelea kujenga
mahusiano ya karibu na mashirika mbalimbali ya kimataifa kama vile Benki
ya Dunia; mashirika yasiyo ya kiserikali yenye nguvu za kiuchumi na
kisiasa; na makampuni ya kimataifa ya mafuta, nishati, mawasiliano na
miundombinu ili kupata mitaji na teknolojia inayohitajika nchini kwetu.
Kusimamia Mikataba na Makubaliano ya Kimataifa
36. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016Wizara iliratibu na kusimamia uwekwaji saini wa mikataba ifuatayo:-
(a) Hati
za Makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Serikali za Sri – Lanka, Serbia, Ghana, Malta, Qatar, Kuwait na Morocco
kuhusu masuala ya Usafiri wa Anga yaliyotiwa saini mwezi Oktoba, 2015;
(b) Hati
ya Makubaliano kati ya Wizara na Taasisi ya Maendeleo ya Miundombinu
kuhusu kuendeleza viwanja na nyumba zinazomilikiwa na Serikali nje ya
nchi, uliowekwa saini tarehe 08 Desemba, 2015 – Dar es Salaam;
(c) Mkataba
wa Uenyeji kati ya Tanzania na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kuhusu
Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki
yaliyoko Zanzibar. Mkataba huo uliwekwa saini tarehe 28 Desemba, 2015; na
(d) Mkataba
wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Ufalme wa Saudi Arabia katika nyanja
za uchumi, biashara, uwekezaji, michezo na vijana uliosainiwa tarehe 24
Machi, 2016.
37. Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kufuatilia utekelezaji wa mikataba hiyo ili kusimamia maslahi ya nchi.
Kuratibu Masuala ya Uhusiano baina ya Tanzania na nchi mbalimbali, Ushirikiano wa Kimataifa, Bara la Afrika na Kikanda
Ushirikiano wa Kimataifa
Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030
38. Mheshimiwa Spika, mwaka
2015 utakumbukwa sana na Jumuiya ya Kimataifa kutokana na makubaliano
na maamuzi muhimu ya kimataifa yaliyofikiwa. Miongoni mwa makubaliano
hayo ni kupitishwa kwa Ajenda Mpya ya Maendeleo kwenye Mkutano Maalum
wa Umoja wa Mataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika New York,
Marekani mwezi Septemba, 2015. Katika Mkutano huo, viongozi hao
walikubaliana kuwa na dira mpya ya maendeleo ya dunia ijulikanayo kama
Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 yenye jumla ya Malengo 17 na
shabaha 169. Ajenda hii mpya ya maendeleo endelevu inarithi Malengo ya
Maendeleo ya Milenia ya miaka 15 yaliyomalizika mwaka 2015.
39. Mheshimiwa Spika, malengo
hayo yamejikita katika kutokomeza umaskini; kuhifadhi mazingira;
kupambana na mabadiliko ya tabianchi; na kushirikisha makundi yote
kwenye jamii katika masuala ya maendeleo. Ninajivunia kuwa Tanzania
ilitoa mchango mkubwa sana katika ngazi mbalimbali kipindi chote cha
majadiliano yaliyopelekea kupatikana kwa malengo hayo na hivyo
kuhakikisha kuwa vipaumbele vya nchi vinakuwepo kwenye Ajenda hiyo mpya
ya Maendeleo. Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa nchi 30 zilizounda
Kikundi Kazi kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu ambacho ndicho
kilichopendekeza malengo hayo.
40. Mheshimiwa Spika, utekelezaji
wa Malengo hayo umeanza rasmi mwezi Januari mwaka huu na napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa malengo hayo yameshaingizwa kwenye
mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi ili kuendana na vipaumbele vyetu
hasa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/2017 -
2020/2021) uliowasilishwa kwenye Bunge lako Mwezi Aprili 2016 na Waziri
wa Fedha na Mipango.
41. Mheshimiwa Spika, inazidi
kubainika katika Jumuiya ya Kimataifa kuwa moja ya vikwazo vikubwa vya
maendeleo ni rushwa na ufisadi. Uongozi wa Awamu ya Tano umezidi
kutambulika duniani na kusifiwa kwa ujasiri wa kupambana na janga la
rushwa. Tanzania ilikuwa moja ya nchi na mashirika makubwa 40 duniani
yaliyokaribishwa na Mheshimiwa David Cameroon, Waziri Mkuu wa Uingereza
kushiriki Mkutano uliojadili juu ya mkakati mpya wa pamoja duniani wa
kupambana na rushwa. Mkutano huo ulifanyika London, Uingereza mwezi Mei,
2016 ambapo Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, alimwakilisha Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika
Mkutano huo, Mheshimiwa Majaliwa alipata nafasi ya kufafanua hatua
mbalimbali za kisiasa, kisheria na utawala ambazo Serikali ya Tanzania
inachukua katika kupambana na tatizo hilo sugu la rushwa na pia
kuonyesha ushirikiano wa kitaifa katika kuimarisha juhudi hizo.
Usimamizi wa Amani Duniani
42. Mheshimiwa Spika, miongoni
mwa masuala yanayoiletea heshima kubwa nchi yetu ni suala la ulinzi na
utetezi wa amani na usalama kwenye ukanda wetu na sehemu mbalimbali
duniani. Hadi sasa Tanzania imepeleka askari, wanawake kwa wanaume zaidi
ya 2,328 kwenye misheni saba tofauti za kulinda amani za Umoja wa
Mataifa na bado tunaendelea kufanya hivyo. Tunayafanya yote haya kwa
kuwa tunaamini amani ndiyo msingi wa maendeleo na ustawi wa binadamu.
Pia, tunatimiza wajibu wetu kama sehemu ya Jumuiya ya Kimataifa katika
kuhakikisha kuwa dunia inakuwa sehemu nzuri na salama ya kuishi.
43. Mheshimiwa Spika,
Taifa linajivunia sana Askari wetu wanaofanya kazi hizo za kulinda
amani kwani pamoja na kushambuliwa mara kadhaa, wamekuwa wakiifanya kazi
hiyo kwa umahiri, kujitoa, bidii na weledi mkubwa. Ndiyo maana
haishangazi kuona Watanzania mbalimbali wakiwa wanateuliwa kushika
nyadhifa za juu kwenye misheni hizo za kulinda amani. Ninatoa pongezi za
pekee kwa askari wetu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Polisi na raia
walioshiriki kwa vipindi mbalimbali katika vikosi vya kulinda amani vya
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
44. Mheshimiwa Spika,
pamoja na kazi nzuri inayofanywa na askari hawa wazalendo, hivi
karibuni tumepokea tuhuma kwamba baadhi ya askari wetu wamehusika
kudhalilisha kijinsia wanawake huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Tanzania ilizichukulia tuhuma hizi kwa uzito mkubwa sana na iliunda timu
ya uchunguzi kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania ndani ya siku tano
badala ya siku kumi zinazotakiwa na Umoja wa Mataifa baada ya Nchi
husika kupokea taarifa za tuhuma. Tuhuma hizi zimeisikitisha sana
Serikali na endapo zitathibitika hatua kali za kinidhamu dhidi ya wale
wote waliohusika zitachukuliwa. Ili kuhakikisha kuwa vitendo kama hivyo
vinaepukwa siku zijazo, Tanzania itajiunga na kusimamia kikamilifu “Kigali Principles” ambazo ni mwongozo wa jumla kwa nchi zinazopeleka askari wa kulinda amani kwenye vikosi vya Umoja wa Mataifa.
45. Mheshimiwa Spika, maendeleo
ya kisayansi na teknolojia yamesababisha kuongezeka kwa hali ya
uhatarishi kutokana na mbinu za kiuhalifu zinazotumiwa na wahalifu wenye
mitandao ya kimataifa. Mathalan, tumeshuhudia ongezeko la tishio la
ugaidi Afrika Mashariki, biashara haramu ya dawa za kulevya, uvuvi
haramu katika Bahari ya Hindi na mzunguko wa silaha ndogondogo. Wizara
yangu kupitia Jumuiya za Kikanda na Kimataifa na ushirikiano tulionao na
nchi zilizondelea, tunaratibu jitihada za kitaifa za kukabiliana na
uhalifu wa kimataifa. Kwa mfano, kupitia Mkutano wa Baraza la Mawaziri
wa Nchi Wanachama wa SADC uliofanyika Gaborone, Botswana mwezi Agosti,
2015 Nchi Wanachama zilikubaliana kuandaa Mkakati wa SADC wa kukabiliana
na Ugaidi, Mkakati wa SADC wa kukabiliana na ujangilina Mkakati wa SADC wa kukabiliana na uzagaaji wa silaha ndogondogo.
46. Mheshimiwa Spika,
katika kuendeleza jitihada za kupambana na uharamia baharini, Wizara
iliratibu ushiriki wa Serikali katika Mkutano wa Tatu wa Majadiliano ya
Bahari ya Hindi uliofanyika mwezi Machi, 2016 nchini Indonesia. Pamoja
na mambo mengine, Mkutano huo ulijadili changamoto zinazoukabili Ukanda
huo ikiwemo vitendo vya uharamia, uhalifu wa kutumia silaha,
usafirishaji haramu na ugaidi wa majini ambavyo vinaathiri maendeleo ya
uchumi. Kutokana na kuwepo kwa changamoto hizo, Mkutano ulifikia
Makubaliano yajulikanayo kama Padang Consensus yanayozitaka Nchi
Wanachama kuandaa mikakati mbalimbali kwa kutumia sheria za kimataifa
zilizopo katika kupambana na vitendo hivyo haramu. Tanzania imejipanga
kutekeleza makubaliano hayo kupitia Kamati ya Kitaifa ya Usalama Majini
iliyo chini ya Uenyekiti wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na
Nchi Kavu.
47. Mheshimiwa Spika, Tanzania
ni mhanga wa biashara haramu ya silaha ndogondogo kutokana na
kuzungukwa na nchi zenye machafuko hasa kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu.
Kutokana na kuwepo kwa hali hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali imekuwa ikichukua hatua madhubuti za kukabiliana na
changamoto hiyo ikiwemo kutunga sheria na kanuni za kudhibiti biashara
hiyo haramu; kuweka alama silaha zinapoingizwa nchini na kuzisajili; na
kuchoma silaha haramu. Jitihada hizi pia zinafanyika kimataifa ikiwemo
kusaini mikataba mbalimbali kama vile Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti
Biashara ya Silaha. Aidha, jitihada hizi zinapewa nguvu zaidi na lengo
la 16 la Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu ambalo linazitaka nchi
kupunguza ufadhili na usambazaji haramu wa silaha ndogondogo ifikapo
mwaka 2030.
Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Paris
48. Mheshimiwa Spika, katika
miaka ya hivi karibuni tumekuwa mashuhuda wa athari za mabadiliko ya
Tabianchi yanayosababisha kuwepo kwa ongezeko la ukame; mvua nyingi
zinazoleta mafuriko; kuzama kwa baadhi ya visiwa; vimbunga na tufani
kubwa; kupotea kwa baadhi ya mimea na wanyama na kuongezeka kwa kina cha
bahari. Hali hii sio tu inapoteza maisha ya binadamu wengi na mali zao,
bali pia inaturudisha nyuma kwenye jitihada zetu za maendeleo na
kutokomeza umaskini. Ni kwa msingi huo, Tanzania kama ilivyo nchi nyingi
zinazoendelea imeunga mkono kupatikana kwa Mkataba mpya unaolenga
kudhibiti mabadiliko ya tabianchi. Mkataba huo ulikubaliwa wakati wa
Mkutano wa 21 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi
uliofanyika Paris, Ufaransa mwishoni mwa mwaka 2015. Mkataba huo tofauti
na mingine iliyopita una mamlaka ya kisheria kuzibana nchi
zilizoendelea na zenye viwanda vingi kupunguza gesijoto.
49. Mheshimiwa Spika, Mkataba
huo uliokubaliwa na nchi zote, ulitiwa saini tarehe 22 Aprili, 2016
kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York na nchi 175 zikiwemo
zile kubwa ambazo zilikuwa zikipinga Mikataba iliyopita. Tanzania
ilikuwa ni miongoni mwa nchi zilizotia saini Mkataba huo. Naomba
nichukue fursa hii kuzisihi nchi zote hasa zile zilizoendelea na
zinazotoa gesijoto kwa wingi kuheshimu makubaliano hayo ili kupunguza
athari za mabadiliko ya tabianchi na kuitunza dunia yetu kwa manufaaa ya
vizazi vya sasa na vijavyo. Aidha, ninawaasa Watanzania wote kulinda misitu yetu, uoto asilia na wanyamapori wetu kwa manufaa ya Taifa letu.
50. Mheshimiwa Spika, sitaweza
kuhitimisha hoja hii ya Mkataba wa Paris bila kumpongeza binti wa
Kitanzania, Getrude Clement, mwenye umri wa miaka 16 ambaye alipata
nafasi ya kulihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa niaba ya vijana
duniani wakati wa hafla ya utiaji saini Mkataba huo. Ninaona fahari
kuwa nafasi hiyo alipewa mtoto wa Kitanzania miongoni mwa vijana wengi
duniani kutokana na uwezo mkubwa alionao. Binti huyo ameliletea heshima
Taifa na napenda kutumia nafasi hii kuwasihi watoto na vijana wengine
hapa nchini kuweka jitihada kwenye masomo na shughuli zao wanazozifanya
ili siku moja nao wapate nafasi kama hizi na kupeperusha vizuri bendera
ya Taifa. Mtoto huyu awe mfano kwa kizazi kipya cha Watanzania ambao watakuwa makini katika kulinda urithi wa mazingira yetu.
Uteuzi wa Watanzania kwenye Mashirika na Taasisi za Kimataifa
51. Mheshimiwa Spika, kutokana
na mahusiano mazuri tuliyonayo na nchi nyingine, Watanzania wameendelea
kupewa nafasi muhimu kwenye mashirika na taasisi za kimataifa. Suala
linalozidi kuipa sifa nchi yetu na kuthibitisha imani iliyowekwa na
Jumuiya ya Kimataifa kwa nchi hii na watu wake.
52. Mheshimiwa Spika, napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa mwezi Februari 2016, Mhe. Samia Suluhu
Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteuliwa
na Bw. Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa mmoja wa
wajumbe wa Jopo la Ngazi za juu la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa kuhusu Masuala ya Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi. Aidha, mwezi Januari 2016,Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania aliteuliwa kuwa Mwakilishi wa Umoja wa Afrika kwenye utatuzi wa
mgogoro wa Libya. Uteuzi wa Mhe. Kikwete unalenga kusaidia juhudi za
Umoja wa Afrika katika kurejesha amani na utulivu nchini Libya kwa
kutumia uzoefu wake. Pia katika mwezi huo wa Januari, Mhe. Kikwete, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mwenza wa Jopo la Watu Mashuhuri la Umoja wa Mataifa lenye jukumu la kutoa
mwongozo wa agenda ya kina mama na watoto wakati huu wa mpito kutoka
Malengo ya Milenia kwenda Malengo ya Maendeleo Endelevu.
53. Mheshimiwa Spika, uteuzi
haukuishia tu kwa viongozi hawa wa Kitaifa, Watanzania wengine pia
wameendelea kuchaguliwa na kuteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali kubwa
kwenye Mashirika na Taasisi za Kimataifa. Hawa ni pamoja na Dkt.
Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani; Bw.
Gabriel Rugalema ambaye ameteuliwa kuwa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la
Chakula na Kilimo Duniani nchini Sierra Leone; Profesa Kennedy Gastorn
ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Kitivo cha Sheria,
alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mashauriano ya Masuala ya
Kisheria katika nchi za Asia na Afrika nafasi ambayo ataanza kuitumikia
mwezi Agosti 2016; na Balozi Wilfred Ngirwa alichaguliwa kuendelea na
nafasi yake ya Mwenyekiti Huru wa Baraza la Shirika la Chakula na Kilimo
Duniani. Pia, Bw. Donatius Kamamba, alichaguliwa kuwa Mjumbe kwenye
Kamati ya Urithi wa Dunia ya Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni na Dk. Frannie Leautier
alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Kuratibu Masuala ya Ushirikiano Barani Afrika
Umoja wa Afrika
54. Mheshimiwa Spika, Wizara
kwa kushirikiana na Ubalozi wetu wa Addis Ababa, Ethiopia, imeendelea
kuratibu ushiriki wa Tanzania katika shughuli mbalimbali za Umoja wa
Afrika. Mwezi Januari 2016, Tanzania ilishiriki kwenye Mkutano wa 26 wa
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa,
Ethiopia. Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo.
Kaulimbiu ya mkutano huo ilikuwa ni “Mwaka wa Haki za Binadamu Afrika, hususan Haki za Wanawake”. Wakati
wa uzinduzi wa kaulimbiu hiyo, Nchi Wanachama zilihimizwa kuridhia na
kutekeleza Itifaki na sera mbalimbali zilizoundwa na Umoja huo kwa lengo
la kulinda, kukuza na kutekeleza haki za wanawake Afrika. Itifaki hizo
ni pamoja na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na Sera ya
Umoja wa Afrika kuhusu Masuala ya Jinsia. Mkutano huo pamoja na masuala
mengine pia ulijadili ripoti ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa
Afrika kuhusu hali ya amani na usalama Barani Afrika.
55. Mheshimiwa Spika, mwezi
Novemba, 2015 Tanzania iliteuliwa na Umoja wa Afrika kusimamia uzinduzi
wa Jeshi la Pamoja la Afrika la Kulinda Amani Barani Afrika. Mimi
mwenyewe nilisimamia uzinduzi huo. Tanzania
vilevile iliendelea kutoa mchango wake katika kutafuta suluhu ya
migogoro barani Afrika. Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, ilieleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Jumuiya ya
Afrika Mashariki katika kutatua mgogoro wa Burundi. Mchango wa Tanzania
katika Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro wa Burundi kwa kiasi kikubwa
uliweza kusaidia Umoja huo kuwa na taswira mpya ya namna ya kutafuta
suluhu ya kudumu ikiwemo kutoa kipaumbele katika mazungumzo
yanayohusisha pande zinazohasimiana nchini Burundi chini ya usimamizi wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki badala ya uamuzi wa awali wa kupeleka
majeshi ya Umoja huo nchini Burundi.
56. Mheshimiwa Spika,
napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba Tanzania ilichaguliwa
kuwa mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kwa vipindi
viwili mfululizo kuanzia mwaka 2012 hadi mwezi Januari, 2016. Hii
inatokana na mchango wake mkubwa katika kusuluhisha migogoro barani
Afrika. Katika uchaguzi wa wajumbe wapya wa Baraza hilo uliofanyika
mwezi Januari 2016, Kenya, Rwanda na Uganda zilichaguliwa kuwakilisha
ukanda wa Afrika Mashariki.
Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano kati ya Afrika na India
57. Mheshimiwa Spika, Wizara
pia iliratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano wa Tatu wa
Ushirikiano kati ya Afrika na India, uliofanyika New Delhi, India mwezi
Oktoba, 2015. Katika Mkutano huo, pamoja na masuala mengine, India
iliahidi kuisaidia
Afrika katika kuendeleza miundombinu; umwagiliaji; kuongeza thamani ya
rasilimali; kuanzisha viwanda; na teknolojia ya habari na mawasiliano.
Aidha, Serikali ya India iliahidi kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa
Dola za Marekani bilioni 10, ruzuku ya misaada ya Dola za Marekani
milioni 600 na kuchangia Dola za Marekani milioni 100 kwa ajili ya Mfuko
wa Maendeleo. Vilevile, India iliahidi kutoa nafasi 50,000 za ufadhili
wa masomo kwa wanafunzi wa Afrika nchini India kwa miaka mitano ijayo.
Ili kunufaika na fursa hizi, nchi za Afrika zinatakiwa kuwasilisha
andiko la miradi mbalimbali ya vipaumbele kwa Serikali ya India.
58. Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kufuatia mkutano huo, tayari Serikali
imeandaa na kuwasilisha miradi ya kipaumbele ikiwemo miradi 17 ya maji
pamoja na Mradi wa Serikali Mtandao. Aidha, miradi mingine
itakayowasilishwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa atamizi kwa ajili ya
viwanda vidogo na vya kati katika kila mkoa; mradi wa ujenzi wa reli
itakayotumika kusafirisha abiria katika Jiji la Dar es Salaam; na mradi
wa kilimo cha umwagiliaji – Zanzibar.
Mkutano wa Sita wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika
59. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu na kushiriki Mkutano wa Sita wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwezi Desemba
2015, Jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Katika
mkutano huo Serikali ya China ilitangaza mpango mpya wa miaka mitatu
kuanzia 2016 hadi 2018 wa ushirikiano kati ya China na Afrika ambao
umeweka kipaumbele katika kuendeleza sekta ya viwanda barani Afrika.
Tanzania ni miongoni mwa nchi nne za mfano zilizochaguliwa na China kwa
ajili ya kujenga viwanda vya mfano. Nchi nyingine zilizomo kwenye mpango
huo ni Afrika Kusini, Ethiopia na Kenya.
60. Mheshimiwa Spika, kupitia
Mpango huo, Serikali ya China imetangaza kutenga Dola za Marekani
bilioni 10 kwa ajili ya kuendeleza sekta ya viwanda barani Afrika.
Aidha, China itatoa nafasi 40,000 za mafunzo ya kuwajengea waafrika
stadi za ufundi nchini China na nafasi 200,000 kwenye nchi zao; kutuma
wataalam wa China katika nchi za Afrika kwa ajili ya kutoa ushauri wa
namna ya kutekeleza programu ya viwanda; na kujenga vyuo vya ufundi vya
kikanda kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa viwandani.
61. Mheshimiwa Spika, ili kunufaika na Mpango huo, Serikali ya Tanzania imebainisha na kuwasilisha miradi ya kipaumbele ambayo ni Ujenzi wa Reli ya Kati katika kiwango cha kimataifa; ujenzi wa miundombinu wezeshi ya reli, barabara, kina cha bandari, umeme, gesi na maji katikaUkanda Maalum wa Uchumi wa Bagamoyo; Ujenzi wa mtandao wa kusambaza gesi katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Pwani (Bagamoyo na Mkuranga); Upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Abeid Amani Karume – Zanzibar; na Ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri – Zanzibar.
Kuratibu Masuala ya Ushirikiano wa Kikanda
Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu
Mikutano ya Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.
62. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi hiki Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa Mawaziri
wa Sheria wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu
uliofanyika Livingstone, Zambia mwezi Agosti, 2015. Mkutano huo
ulipokea taarifa kutoka Nchi Wanachama kuhusu hatua zilizofikiwa katika
kuridhia na kutekeleza Itifaki za Jumuiya ya nchi za Ukanda wa Maziwa
Makuu hususan Itifaki nne zinazopewa kipaumbele katika utekelezaji wake
kwa sasa. Itifaki hizo ni; Itifaki ya Ushirikiano wa Kiulinzi; Itifaki
ya Ushirikiano wa Kimahakama; Itifaki ya Kuzuia Uvunaji Haramu wa
Maliasili na Itifaki ya Kuzuia Unyanyasaji wa Kijinsia dhidi ya Wanawake
na Watoto. Mkutano huo ulibaini itifaki hizo hazijatekelezwa kikamilifu
na nchi zote wananchama. Hivyo, nchi wanachama zilikubaliana kutekeleza
itifaki hizo kikamilifu.
63. Mheshimiwa Spika, katika
kutekeleza Itifaki hizo Serikali imechukua hatua mbalimbali zikiwemo
kutunga Sheria ya kudhibiti uhalifu wa njia ya mawasiliano; Sheria ya
kurudishiana wahalifu waliokimbilia nchi nyingine; kuanzisha vitengo
maalum katika viwanja vya ndege vya Kimataifa nchini ili kudhibiti
usafirishaji holela wa Maliasili; kuanzisha Mpango wa Mataifa wa
kuwalinda wanawake na watoto dhidi ya unyanyasaji wa kujinsia na
kuanzisha kitengo maalum katika vituo vya polisi Wilaya zote nchini
kushughulikia kesi za uonevu wa kijinsia.
64. Mheshimiwa Spika, Wizara
pia iliratibu ushiriki wa wataalamu wa Tanzania katika Mkutano wa
Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu uliofanyika Luanda, Angola mwezi
Januari, 2016. Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa katika Mkutano
huo ni kutathmini hali ya ulinzi na usalama katika nchi za eneo la
Ukanda wa Maziwa Makuu hususan katika nchi za Burundi, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini. Pamoja na mambo mengine Jumuiya
hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Taasisi za Kikanda katika
kuratibu shughuli za kutatua migogoro. Kwa mfano, mgogoro wa Burundi kwa
kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki, mgogoro wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo kwa kushirikiana na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini
mwa Afrika pamoja na mgogoro wa Sudan Kusini kwa kushirikiana na
Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Nchi za Mashariki na Pembe ya
Afrika.
65. Mheshimiwa Spika, Jumuiya
hiyo ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ambayo Tanzania ni mwanachama
inatambua uhusiano mkubwa uliopo kati ya uvunaji haramu wa rasilimali na
kushamiri kwa migogoro. Hivyo, nchi wanachama zimesaini Itifaki ya
Ulinzi, Usalama na Maendeleo pamoja na Itifaki ya Kupinga Uvunaji Haramu
wa Rasilimali ambazo kwa pamoja zinazitaka nchi zote 12 wanachama kutii
taratibu zinazotambulika kikanda za uvunaji rasilimali ambapo Cheti ya
Kikanda cha kuthibitisha uvunaji huo hutolewa. Hii kwa kiasi kikubwa
imesaidia kudhibiti makundi ya waasi kujipatia fedha kwa njia za uvunaji
haramu wa rasilimali kwa lengo la kufadhili shughuli zao.
66. Mheshimiwa Spika, jitihada
hizo za pamoja zimepelekea kutengamaa kwa hali ya ulinzi na usalama
katika nchi za maziwa makuu. Kwa mfano, idadi ya wakimbizi wanaoingia
nchini imepungua kutoka kati ya wakimbizi 200 hadi 300 kwa siku kwa
mwezi Novemba, 2015 hadi kufikia wakimbizi kati ya 100 hadi 120 kwa siku
kwa mwezi Mei, 2016. Hadi sasa Tanzania inahifadhi jumla ya wakimbizi
136,000 kutoka Burundi na wengine 2,360 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo. Bado idadi hii ni kubwa na Serikali inaendelea kushirikiana na
wadau wengine katika jitihada za kutatua migogoro katika ukanda wetu wa
Maziwa Makuu ili hatimaye wakimbizi hao waweze kurejea nchini mwao.
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
67. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na
Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika mwezi
Agosti 2015 Gaborone, Botswana. Mkutano huo ulijadili masuala ya siasa, uchumi, uwekezaji, kijamii, ulinzi na usalama katika Kanda.
68. Mheshimiwa Spika, pamoja na Mkutano
huo kuiteua Tanzania kuwa Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi
na Usalama wa Jumuiya hiyo, Nchi Wanachama ziliazimia yafuatayo:-
i. Serikali
ya Lesotho pamoja na washirika wengine wa kisiasa nchini humo kuandaa
mapema iwezekanavyo mpango wa utekelezaji wa mabadiliko ya Katiba na
Sekta ya Ulinzi;
ii. Kuhakikisha
kuwa kunakuwepo na ongezeko la uwakilishi wa wanawake katika nafasi
mbalimbali za maamuzi ya juu Serikalini na sekta binafsi;
iii. Kutekeleza
kikamilifu Sera ya Kilimo ya Kanda na Itifaki zingine ili kusaidia
kuongeza kasi ya uzalishaji, biashara na ushindani katika sekta ya
kilimo; na
iv. Sekretariati
kufuatilia kwa karibu kwa kushirikiana na Nchi Wanachama kuhakikisha
UKIMWI na magonjwa mengine ya kuambukiza hayaendelei kuwa tishio kwenye
Sekta ya Afya katika Kanda.
69. Mheshimiwa Spika, kutokana na nchi
yetu kujijengea sifa ya umahiri na weledi katika masuala ya siasa,
ulinzi na usalama barani Afrika na katika Kanda, katika mkutano huo,
Tanzania iliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekitiwa Asasi ya SADC ya
Siasa, Ulinzi na Usalama kwa kipindi cha mwaka 2015/2016. Kutokana na
uteuzi huo, Tanzania kwa mara nyingine itakuwa Mwenyekiti wa Asasi hiyo
katika kipindi cha Agosti 2016 hadi Agosti 2017 ikiwa ni mara ya tatu
kupewa wadhifa huo. Uteuzi
huu unaonyesha imani ya wanachama wa SADC waliyonayo kwa Tanzania
katika kutatua migogoro na kusimamia amani katika kanda hiyo na
unaendelea kuijengea nchi yetu heshima kubwa na kuiweka juu katika
medani za Kikanda na Kimataifa.
Mkutano
wa dharura wa Viongozi Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika wanaosimamia Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama
70. Mheshimiwa Spika,
Tanzania ilishiriki kwenye Mkutano wa Dharura wa Viongozi Wakuu wa Nchi
za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika wanaosimamia Asasi ya Siasa,
Ulinzi na Usalama uliofanyika Gaborone, Botswana tarehe 18 Januari, 2016
kwa ajili ya kujadili hali ya kisiasa nchini Lesotho. Ujumbe
wa Tanzania kwenye Mkutano huo uliongozwa na Mheshimiwa Kassim Majaliwa
Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja
na mambo mengine, Mkutano huo uliielekeza Serikali ya Jamhuri ya
Lesotho kuitoa kwa umma ripoti ya Tume Huru ya Uchunguzi ya SADC na
kuhakikisha kuwa inatekeleza kwa uadilifu mapendekezo yaliyomo katika
taarifa hiyo ili kuboresha hali ya siasa, ulinzi na usalama nchini humo.
Vilevile, Viongozi Wakuu walisisitiza umuhimu wa kusimamia kwa dhati
utekelezaji wa Mikataba yote mitatu ya amani iliyosainiwa kwa ajili ya
kurejesha amani nchini humo. Taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo
yaliyomo katika ripoti hiyo itawasilishwa kwenye Mkutano wa 36 wa Wakuu
wa Nchi na Serikali uliopangwa kufanyika mwezi Agosti, 2016 Mbabane,
Swaziland.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
71. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya
ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambao ulifanyika Gaborone, Botswana mwezi
Machi, 2016. Pamoja
na masuala mengine, Mkutano huo ulijadili hatua ya utekelezaji ya
Mpango wa Kikanda wa Maendeleo 2015 - 2020; hatua ya utekelezaji wa
Mpango wa Kikanda wa Maendeleo ya Viwanda; na Mtangamano wa Utatu wa
Eneo Huru la Biashara la COMESA-EAC-SADC. Mkutano
huo pia ulipokea taarifa ya utekelezaji wa maamuzi ya vikao vya Baraza
la Mawaziri ambayo ilihusisha jumla ya maeneo kumi. Taarifa hiyo
inaonyesha kuwa utekelezaji wa maeneo hayo unaendelea vizuri.
72. Mheshimiwa Spika, Mkutano
huo pia, ulipokea maombi ya Serikali ya Visiwa vya Comoro na Serikali
ya Burundi ya kutaka kujiunga na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika. Hivi
sasa Sekretarieti inaendelea na zoezi la kutathmini maombi ya nchi hizo
kulingana na taratibu, kanuni na sheria za Jumuiya za kuwa mwanachama.
Taarifa ya tathmini hiyo itatolewa kwenye Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi
ambao umepangwa kufanyika mwezi Agosti, 2016, Mbabane, Swaziland.
Jumuiya ya Nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi
73. Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kuwa
mwanachama wa mstari wa mbele katika kuimarisha ushirikiano wa nchi
zilizo katika mwambao wa Bahari ya Hindi kupitia Jumuiya ya Nchi hizo.
Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri kuhusu ‘Blue Economy’
74. Mheshimiwa Spika, Wizara ilishiriki katika Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi kuhusu Blue Economy uliofanyika mwezi Septemba, 2015 nchini Mauritius. Mkutano huo ulijadili maeneo manne ya kipaumbele kuhusu matumizi endelevu ya rasilimali zitokanazo na bahari. Maeneo hayo ni Fisheries and Aquaculture;Renewable Ocean Energy; Seaport and Shipping; na Seabed Exploration and Minerals.
Mkutano huo pia ulidhamiria kuunda mifumo madhubuti yenye Sera, Sheria
na Mikakati ya Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Bahari na kusimamia
Dhana ya Uchumi wa Bahari ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu
kwa Nchi Wanachama.
75. Mheshimiwa Spika,
katika kutekeleza maazimio ya mkutano huo, Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi
wa Bahari Kuu kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania
inaendelea kufanya utafiti wa kutambua maeneo yenye samaki wengi hususan
aina ya Jodari pamoja na majaribio ya kuweka vifaa vya kuvutia samaki
katika Bahari ya Hindi. Utafiti huu unaohusisha maeneo ya Mafia,
Zanzibar na Bagamoyo unalenga kuwapunguzia wavuvi muda wa kutafuta
samaki, kupunguza gharama za mafuta na kuwaongezea kipato. Vilevile,
taarifa za utafiti huo zitatolewa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi
ili waje kuwekeza katika uvuvi wa Bahari Kuu ya Tanzania.
Kulinda na kuendeleza Maslahi ya Taifa ya Kiuchumi na Mengineyo nje ya nchi
Mkutano wa 70 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
76. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu na kushiriki kwenye Mkutano wa 70 wa Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa uliofanyika New York, Marekani, mwezi Septemba, 2015 ambapo
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania alipata nafasi ya kulihutubia Baraza hilo na
kueleza msimamo wa nchi kwenye masuala mbalimbali duniani, yakiwemo ya
kiuchumi na maendeleo, amani na usalama, pamoja na mahusiano yetu na
nchi nyingine. Aidha, Mheshimiwa Kikwete alifanya mazungumzo na nchi
marafiki na washirika wetu wa maendeleo na kukubaliana masuala
mbalimbali yenye manufaa kwa nchi ikiwemo ufadhili wa miradi ya
maendeleo.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola
77. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu na kushiriki kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Jumuiya ya Madola uliofanyika Malta mwezi Novemba, 2015. Tanzania
ilishiriki kikamilifu kwenye majadiliano mbalimbali yaliyofanyika na
hivyo tamko la mwisho ya mkutano liliakisi maslahi ya nchi hususan
kwenye masuala ya amani na usalama; haki za binadamu na utawala bora;
maendeleo endelevu; mabadiliko ya tabianchi; biashara na usawa wa
kijinsia na kumwezesha Mwanamke.
78. Mheshimiwa Spika, kwa
mara ya kwanza baada ya miaka 66, Jumuiya ya Madola ilimchagua mwanamke
mwenye asili ya Afrika, Mheshimiwa Baroness Patricia Scotland mzaliwa
wa Dominica na mwenye uraia pacha wa Dominica na Uingereza kuwa Katibu
Mkuu wa sita wa Jumuiya hiyo ambapo alianza kazi tarehe 1 Aprili, 2016.
Vipaumbele alivyoainisha Mheshimiwa Scotland ni pamoja na kushughulikia
unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto wa kike; athari za mabadiliko ya
Tabianchi; biashara na utawala bora; na kuanzisha majadiliano na nchi
wanachama kuhusu kutokufanya suala la mahusiano/mapenzi ya jinsia moja
kuwa kosa la jinai. Alisisitiza kuwa nchi haziwezi kulazimishwa kufuata
suala hili lakini ataanzisha majadiliano na lazima pawepo na makubalino
ya pande zote. Wizara itaendelea kufuatilia kwa makini ajenda zake ili
kuhakikisha masuala ambayo yanapingana na sheria, mila na desturi za
nchi yetu hayawi sehemu ya majadilino ya Jumuiya.
Mkutano wa 10 wa Nchi Wanachama wa Shirika la Biashara Duniani
79. Mheshimiwa Spika, Wizara
pia iliratibu na kushiriki kwenye Mkutano wa 10 wa Mawaziri wa Nchi
Wanachama wa Shirika la Biashara Duniani uliofanyika mwezi Desemba 2015,
Nairobi, Kenya. Katika Mkutano huo Tanzania ilitetea maslahi yake hasa
kuhusu masuala ya biashara ya kilimo na mazao yake ikiwemo pamba kwa
kushirikiana na makundi ya Afrika; Nchi Masikini zaidi Duniani; Kundi la
77 na China; na Kundi la Afrika, Karibiani na Pasifiki, hivyo kuwa na
ushawishi kwenye matokeo ya Mkutano huo yanayojulikana kama Nairobi Package. Makubaliano yaliyofikiwa kwenye Mkutano huo ni pamoja na nchi zilizoendelea kusitisha ruzuku ya kuuza nje mazao ya kilimo na kuimarisha soko kwa nchi zinazoendelea. Makubaliano haya ni muhimu zaidi kuwahi kufanyika ndani ya miaka 20 ya uhai wa Shirika hilo.
Ushiriki wa Watanzania waishio Ughaibuni katika Maendeleo ya Nchi
80. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea na juhudi za kuwahamasisha na kuwashirikisha Diaspora wa
Tanzania waishio maeneo mbalimbali duniani katika kuchangia maendeleo ya
nchi yetu. Jitihada hizo zimeleta mafanikio katika nyanja za uwekezaji,
biashara na kubadilishana uzoefu, elimu na ujuzi. Diaspora waliopo
katika nchi mbalimbali kama vile, Australia, Botswana, Marekani, Oman na
Thailand wamekuwa mstari wa mbele katika kutafuta fursa za biashara,
elimu pamoja kuutangaza utalii wa nchi yetu. Kwa mujibu wa takwimu
zilizokusanywa kupitia Balozi zetu, Watanzania waishio nje ya nchi
wanakadiriwa kuwa zaidi ya milioni moja kote duniani. Kitaaluma wapo
Wahandisi, Madaktari, Wachumi, Wahadhiri na Wakufunzi katika nyanja
mbalimbali na pia wafanyabishara; ambao wote hawa wametawanyika sehemu
mbalimbali duniani.
81. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu na kushiriki katika Kongamano la Pili la Diaspora
lililofanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Agosti, 2015. Lengo la
Kongamano hilo lilikuwa ni kuhamasisha Diaspora kushiriki katika kukuza
sekta ya biashara ndogondogo na za kati na kuboresha mahusiano kati ya
Diaspora na Wajasiriamali waliopo nchini. Aidha, Wizara imeendelea
kuratibu makongamano mengine ya kibiashara na uwekezaji yanayofanyika
nje ya nchi kama yale yanayoandaliwa na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi
nchini Marekani.
82. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu ziara ya kitabibu ya Madaktari Watanzania kwa kushirikiana na
madaktari wenzao wa kiafrika waishio nchini Marekani mwezi Julai 2015.
Madaktari hao walitoa huduma za matibabu na ushauri katika hospitali za
Mwananyamala (Dar es Salaam) na Mnazi Mmoja (Zanzibar) kwa magonjwa ya
moyo, saratani na kinywa. Aidha, walitoa msaada wa madawa na vifaa tiba
vyenye thamani ya Dola za Marekani 300,000 kwenye hospitali hizo na
kukabidhi mashine ya kupima saratani ya matiti yenye thamani ya Dola za
Marekani 200,000 katika Hospitali ya Lugalo.
83. Mheshimiwa Spika, naomba
kutumia nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru madaktari hao kwa moyo
wao wa dhati wa kujitolea. Aidha, ningependa kuwahamasisha Diaspora
wengine kuiga mifano hiyo. Wizara yangu iko tayari kushirikiana nao
wakati wote.
84. Mheshimiwa Spika, napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa katika kuitikia wito wa kuchangia
maendeleo ya nchi yetu, uwekezaji wa Diaspora katika Benki ya CRDB,
Mfuko wa Pensheni wa PSPF na Mfuko wa Mitaji wa UTT umefikia Shilingi
Bilioni 26 mwaka 2015. Aidha, uwekezaji wa Diaspora katika mifuko
mingine ya hifadhi za jamii, sekta za afya, viwanda na utalii
umeongezeka.
85. Mheshimiwa Spika, katika
kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira wezeshi kwa Diaspora, Wizara
yangu imekamilisha hatua za awali za kutengeneza Sera ya Diaspora kwa
ushirikiano na Mfuko wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na
Pasifiki. Sera hii itatoa mwongozo kwa wadau na kuleta uelewa wa pamoja
kuhusu mikakati bora ya kuwatambua Diaspora na kuwawezesha kuchangia
maendeleo ya nchi. Rasimu ya Sera hiyo itawasilishwa kwa wadau kwa ajili
ya maoni na ushauri. Ni matarajio ya Serikali kuwa ushirikishwaji wa
Diaspora kama moja ya wadau wa maendeleo utawawezesha kuchangia katika
maendeleo ya nchi yetu kwa kuleta teknolojia mpya; na kuongeza uwekezaji
kwenye sekta mbalimbali kama vile viwanda, masoko ya mitaji, kilimo na
utalii. Ushirikishwaji huo wa Diaspora utaiwezesha nchi kufikia malengo
ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
86. Mheshimiwa Spika, Wizara
kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania na wadau wengine
inaandaa mfumo sahihi wa kutambua na kurahisisha uingiaji wa fedha
kutoka kwa Diaspora ili kuwa na takwimu sahihi za mchango wa Diaspora
kwenye kuongeza Pato la Taifa.
Kusimamia
masuala yanayohusu Kinga na Haki za Kibalozi kwa Wanadiplomasia waliopo
nchini kulingana na Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961
87. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kushirikiana na mamlaka mbalimbali nchini ili kuhakikisha
kuwa, jamii ya wanadiplomasia waliopo nchini wanapata haki zao kama
ilivyoainishwa katika Mkataba wa Vienna Kuhusu Mahusiano ya Kidiplomasia
wa mwaka 1961. Wizara inasimamia kikamilifu utekelezaji wa Mkataba huo
kwenye vipengele muhimu vya kinga na haki za kibalozi na wategemezi
wao. Pamoja na jamii ya kibalozi kuwa na kinga na upendeleo maalum,
Wizara inahakikisha kuwa jamii hizi zinaheshimu na kufuata sheria,
kanuni na taratibu za nchi yetu.
88. Mheshimiwa Spika, mara baada ya kuundwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano, nilikutana na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa waliopo nchini. Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, nilitumia
fursa hiyo kuwapatia taarifa ya masuala mbalimbali yanayohusu umuhimu
wa ushirikiano wa Tanzania na nchi nyingine na kutoa Dira ya Serikali ya
Awamu ya Tano. Wizara yangu itaendelea kuwa na vikao vya mara kwa mara
na wanadiplomasia hawa kwa lengo la kuimarisha zaidi ushirikiano.
89. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu ziara za Viongozi wa Kitaifa wa Awamu ya Nne nje ya nchi
ambao ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Makamu
wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Baadhi ya ziara za
Viongozi hao zilifanywa katika nchi za Uswisi, Australia, Marekani,
Misri, India, Kenya, Uganda, Botswana, Vietnam, Uingereza na Italia.
Vilevile, Wizara iliratibu ziara za Viongozi wa Kitaifa wa Awamu ya Tano
nje ya nchi zilizofanyika katika nchi za Afrika Kusini, Botswana,
Ethiopia, Rwanda, Uganda, Uingereza Zambia, Comoro na Papua New Guinea.
90. Mheshimiwa Spika, ziara
hizo zimekuwa na mafanikio ikiwa ni pamoja na kukuza na kuimarisha
mahusiano kati ya nchi yetu na nchi hizo, zimetangaza fursa za
uwekezaji, biashara, utalii na kuwahamasisha Diaspora kuwekeza nyumbani.
Pia zinaimarisha uhusiano kati ya sekta binafsi za hapa nchini na
taasisi mbalimbali za nje.
91. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kufanikishauwasilishaji wa hati
za utambulisho za Mabalozi kutoka nchi mbalimbali. Katika kipindi hiki
Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho ni pamoja na Qutar,
Argentina, India, Denmark, Uswisi, Uturuki, Finland, Sweeden, Ubelgiji,
Hispania, Msumbiji, Uganda, Misri, Israeli, Ufilipino, Jamhuri ya Korea,
Umoja wa Ulaya, Palestina, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya
Namibia, Brazil, Jamhuri ya Czech na Jamhuri ya Sudan Kusini.
Kuanzisha na Kusimamia Huduma za Kikonseli
92. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kutoa huduma za kikonseli kwa kurahisisha upatikanaji wa
viza kwa maafisa na watendaji wa Serikali, Vyama vya Siasa na Taasisi
nyingine zinazostahili huduma hiyo. Aidha, Wizara imeendelea kuratibu
matumizi ya Ukumbi wa Watu Mashuhuri wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere, kwa watu wanaostahili wakiwemo Mabalozi na Wakuu wa
Mashirika ya Kimataifa, viongozi wa Serikali na baadhi ya
Wafanyabiashara hapa nchini. Vilevile, Balozi zetu nje zimeendelea kutoa
Viza kwa raia wa nje wanaoitembelea Tanzania nakushirikiana na mamlaka nyingine kutafuta ufumbuzi wa matatizo mbalimbali yanayowakabili Watanzania waishio nje ya nchi.
93. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kulinda
maslahi ya Watanzania wanaofanya kazi kwenye Balozi mbalimbali na
Mashirika ya Kimataifa hapa nchini. Katika kutekeleza jukumu hilo,
Wizara yangu imebaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya
Watanzania wanaofanya kazi katika Balozi na mashirika hayo kutokuwa na
mikataba ya ajira. Hivyo, natoa rai kwa ofisi za Kibalozi na Mashirika
ya Kimataifa yaliyopo hapa nchini kutoa mikataba kwa waajiriwa wao ili
kukidhi matakwa ya kisheria. Vilevile, nawaasa Watanzania wanaofanya
kazi katika Balozi na Mashirika ya Kimataifa wahakikishe wana mikataba
ya ajira ili kulinda maslahi yao.
94. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kutoa huduma za kikonseli kwa Watanzania waliopo nje ya
nchi. Naomba kutumia fursa hii kuwasihi Watanzania hao kuhakikisha
wanajisajili katika Balozi zetu na Konseli, na pale ambapo hatuna ofisi
za ubalozi wajisajili katika ofisi za ubalozi wa Uingereza kama
ilivyoainishwa kwenye hati za kusafiria.
95. Mheshimiwa Spika, niruhusu
nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla
kwamba miaka ya karibuni pamejitokeza wimbi la Watanzania wanaokwenda
nje ya nchi kwa ahadi za kupatiwa ajira. Kwa upande wa India, Thailand,
Malaysia na China, ahadi hizo za ajira zimekuwa zikitolewa na watu wasio
waaminifu ambao wana mtandao wa biashara ya kusafirisha binadamu.
Mtandao huo unahusisha raia wa Tanzania waliopo ndani na nje ya nchi kwa
kushirikiana na raia wa kigeni waliopo kwenye nchi hizo. Watu hao
wanachofanya ni pamoja na kuwatafuta wasichana wenye umri kati ya miaka
18 na 24, kuwatafutia vibali vya safari na kuwalipia nauli za
kuwafikisha kwenye nchi husika kwa kuwalaghai kuwa wanakwenda kufanya
kazi katika hoteli, migahawa, maduka makubwa au kazi za nyumbani.
Matokeo yake, wanapofika kwenye nchi hizo wasichana hao wanakuta kuwa
ahadi walizo ahidiwa sio za kweli na badala yake wanalazimishwa kukubali
kufanya kazi za ukahaba ili kurejesha fedha walizogharimiwa kufika
huko. Kwa taarifa tulizonazo, mtandao huo wa biashara ya ukahaba
huwataka wasichana hao kurejesha kiasi cha Dola za Marekani kati ya
5,000 hadi 6,000 kiasi ambacho sio rahisi kupata kwa kazi hizo
ikizingatiwa kwamba mapatano na malipo ya kazi hiyo hayafanywi na
wahusika bali madalali wa mtandao huo. Madalali waliowapeleka vijana hao
kwenye nchi hizo huwanyang’anya hati zao za kusafiiria ili kuwadhibiti
wasitoroke hadi kipatikane kiasi cha fedha walizogharimwa. Kwa kuwa
hawana fedha na namna nyingine ya kuishi wasichana hao wamelazimika
kukubali kufanya biashara hiyo.
96. Mheshimiwa Spika, baadhi
ya vijana hao, waliweza kuwatoroka madalali hao, na kukimbilia kwenye
ofisi zetu za Ubalozi kutafuta msaada. Kwa bahati mbaya Mheshimiwa
Spika, Balozi zetu hazina fungu la kuhudumia Watanzania wanaopata shida
ughaibuni na matokeo yake maafisa wa Ubalozi kwa moyo wa kibinadamu
wamekuwa wakitoa fedha zao wenyewe kusaidia kununua tiketi za
kuwarejesha Watanzania waliofanikiwa kuchomoka kwenye makucha ya makuadi
wa ukahaba. Katika jitihada za kukabiliana na tatizo hilo, Wizara imeanzisha mazungumzo na Shirika la Kimataifa la Uhamaji ili wasaidie kuwarudisha nyumbani vijana hao.
97. Mheshimiwa Spika, ni
wazi kwamba vitendo hivyo ni vya kinyama na vinakiuka haki ya binadamu.
Ifahamike pia kwamba usafirishaji wa binadamu ni uhalifu kwa mujibu wa
makosa ya kupangwa ya Azimio la Umoja wa Mataifa NA. 55/25 la mwaka 2003
la kuzuia, kukomesha na kuadhibu usafirishaji wa binadamu hasa kwa
wanawake na watoto chini ya Itifaki yake.
98. Mheshimiwa Spika, Kutokana
na ushirikiano kutoka kwa Jumuiya za Watanzania waishio nchini Thailand
na India, pamoja na baadhi ya wahanga wa biashara hiyo haramu, Serikali
imepata majina ya baadhi ya wahusika wa mtandao huo na tayari
mawasiliano na Serikali za nchi hizo yamefanyika ili kuwakamata wahusika
wote na kuwafikisha katika mkondo wa sheria. Kwa hapa nyumbani,
uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na Balozi za nchi ambazo wasichana
wetu wanapelekwa ili kubaini watu wote walio sehemu ya mtandao huo
hususan wale wanaowezesha upatikanaji wa vibali vya kusafiria kwenye
Balozi hizo ili kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria. Pia
tumeziomba Balozi hizo ziwe makini zaidi kudhibiti uombaji wa vibali vya
kusafiria kwa shughuli mbalimbali na kuwataka wahusika kuthibitisha
uwezo wa kifedha zitakazo wawezesha kutalii, kufanya shughuli ama kuishi
katika nchi wanazokwenda ili kuudhibiti mtandao wa biashara ya watu.
99. Mheshimiwa Spika, Vilevile,
kupitia Bunge hili, ninatoa wito kwa Watanzania wote, tuwe makini pale
tunapopata fursa za kazi nje ya nchi. Kama nilivyosema hapo awali, ni
muhimu kuzingatia na kujiridhisha na masuala yote ya msingi
yanayohusiana na ajira za nje, ikiwa ni pamoja na; kuwepo na mkataba
rasmi wa ajira unaotambuliwa na Mamlaka husika zilizopo nchini na za
Nchi unayotaka kwenda, kujisajili kweye ofisi za Ubalozi wa Tanzania
uliopo katika nchi hizo na kutokubali kuweka hati yako ya kusafiria kama
rehani.
100. Mheshimiwa Spika, nasikitika
kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa bado kuna Watanzania kadhaa
wanatumikia vifungo na wengine kati yao wanakabiliwa na adhabu ya kifo
katika magereza ya nchi mbalimbali duniani baada ya kukutwa na hatia ya
makosa ya kujihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya. Idadi yao
ni kama ifuatavyo: Brazil (41), China (266), Iran (68), India (9),
Nepal (4), Oman (3), Thailand (14) na Umoja wa Falme za Kiarabu (3).
Naomba kuchukua nafasi hii kuwasihi Watanzania kujiepusha na biashara
hiyo kwa kuwa hasara zake ni kubwa kwa familia zao na Taifa kwa ujumla.
Kuratibu shughuli za Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano
101. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kuratibu Mikutano ya Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano
ambazo kimsingi hutoa fursa kwa nchi zetu kujadiliana kwa kina kuhusu
masuala muhimu katika nyanja zote za mahusiano na kuweka mikakati ya
pamoja ya maendeleo.
102. Mheshimiwa Spika, mwezi
Februari 2016, Wizara ilifanya kikao cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya
Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia kilichofanyika hapa nchini. Katika
kikao hicho, pande zote mbili zilikubaliana kuimarisha ushirikiano
katika masuala ya Ulinzi na Usalama Mipakani; kuanzisha Mashauriano ya
Kidiplomasia; Kupunguza Msongamano wa magari katika mpaka wa
Tunduma/Nakonde; na kuanzisha majadiliano ya kutotoza kodi mara mbili
kwenye bidhaa zinazotoka na kuingia katika nchi hizo.
103. Mheshimiwa Spika, Vilevile,
mwezi Aprili 2016, Wizara iliratibu na kushiriki kwenye Kikao kingine
cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda
kilichofanyika Mjini Gisenyi, Rwanda. Katika kikao hicho nchi hizi
zimekubaliana kushirikiana katikakukamilisha
mapema ujenzi wa miundombinu ya ushoroba wa kati kama vile ujenzi wa
reli ya kati katika kiwango cha kimataifa kwa kushirikiana na wadau,
kukuza ushirikiano katika sekta ya anga hususan baina ya Shirika la
Ndege la Rwanda na Shirika la Ndege la Tanzania, kuimarisha ushirikiano
katika sekta za sayansi na teknolojia, afya, kilimo, ufugaji, utalii na
elimu.Mkutano
huo umezidi kuimarisha urafiki na ushirikiano kati ya Tanzania na
Rwanda kufuatia ziara ya kirafiki ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Rwanda mwezi
Aprili, 2016.
104. Mheshimiwa Spika, Wizara imeratibu na kushiriki vikao vya Ujirani Mwema kati ya Tanzania na nchi za Msumbiji, Uganda na Zambia. Vikao hivyo ni muhimu katika kukuza mahusiano katika sekta mbalimbali kati ya Tanzania na nchi husika. Aidha,
Vikao hivyo vinasaidia kutatua matatizo mengi ya mpakani na kurasimisha
biashara baina ya nchi yetu na nchi tunazoshirikiana nazo.
Kusimamia utawala na Maendeleo ya Utumishi Wizarani na kwenye Balozi zetu
105. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi hiki Wizara iliajiri watumishi 42, ambapo maafisa 30 kati ya
hao walipelekwa katika mafunzo maalum ya Jeshi la Kujenga Taifa yenye
lengo la kuwajengea uwezo, uadilifu na uzalendo katika kazi; mtumishi
mmoja alibadilishwa kada; iliwapandisha vyeo watumishi 59; na
iliwathibitisha kazini watumishi 15. Aidha, napenda kuliarifu Bunge lako
Tukufu kuwa, katika kipindi hiki ulifanyika uteuzi wa mabalozi
kuiwakilisha nchi yetu katika nchi za Uholanzi, Malawi, Kuwait, Japan,
Uingereza na Zimbabwe. Vilevile, Wizara imejaza nafasi za Wakurugenzi
zilizokuwa wazi.
106. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kutekeleza mpango wa mafunzo wa miaka mitatu 2013/2014 -
2015/2016. Katika kipindi hiki jumla ya watumishi 43 walihudhuria
mafunzo ndani na nje ya nchi. Kati ya hao, Watumishi 24 walihudhuria
mafunzo ya muda mrefu na watumishi 19 walihudhuria mafunzo ya muda
mfupi. Wizara imeshaanza kuandaa mpango mwingine wa mafunzo wa miaka
mitatu ambao utaanza kutekelezwa kuanzia mwezi Julai 2016 baada ya
mpango wa sasa kuisha muda wake mwezi Juni 2016.
107. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi hiki Wizara imewarejesha nyumbani Mabalozi watano na watumishi
tisa baada ya kustaafu na wengine kumaliza muda wao wa kufanya kazi
Ubalozini. Aidha, Wizara iliwapeleka vituoni Naibu Mabalozi watatu na
watumishi thelathini. Zoezi la kuwarudisha Mabalozi na watumishi
wanaostaafu na wanaomaliza muda wao na kupeleka mbadala wao ni endelevu
na Wizara itaendelea kulitekeleza kadri inavyopata fedha.
TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA
108. Mheshimiwa Spika,
Wizara yangu inasimamia taasisi tatu ambazo ni Chuo cha Diplomasia
kilichopo Kurasini Jijini Dar es Salaam, Mpango wa Kujitathmini
Kiutawala Bora Barani Afrika na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha
Arusha, ambacho pia kinasimamia Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha
Julius Nyerere kilichopo Dar es Salaam.
Chuo cha Diplomasia
109. Mheshimiwa Spika, Chuo kimeendelea kutekeleza
majukumu yake ya kutoa mafunzo, kufanya tafiti, kutoa ushauri wa
kitaaluma na kendesha kozi fupi kwenye nyanja za diplomasia na uhusiano
wa kimataifa. Katika kutekeleza jukumu hilo, Chuo kimejizatiti katika
kutimiza na kutekeleza viwango vilivyowekwa na Baraza la Taifa la
Ithibati la Mafunzo ya Ufundi linalosimamia elimu ya mafunzo na ufundi
kama vile kuwa na wanataaluma wenye vigezo vinavyotambulika, kuboresha
shughuli za kitaaluma, kuboresha majengo na miundombinu ya kitaaluma
pamoja na matumizi ya teknolojia katika taaluma na utawala.
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha
110. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha unaoishia Juni 2015, Kituo kiliweza kuwa mwenyeji wa
mikutano 150 ya kitaifa na 57 ya kimataifa iliyoingiza nchini wageni
wanaokadiriwa kufikia 35,288. Aidha, hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2016
kituo kimeweza kuwa mwenyeji wa Mikutano 82 ambapo 10 ni ya Kimataifa na
72 ya kitaifa.
111. Mheshimiwa Spika,
naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa kwa mara nyingine tena, Kituo
kimeendelea kupata hati safi ya hesabu zake zilizoandaliwa na kukaguliwa
kwa wakati kwa kipindi kilichoishia tarehe 30 Juni, 2015.
112. Mheshimiwa Spika,
Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Kituo kimepanga kuingiza mapato ya
shilingi 15,778,162,803.00 kutokana na vyanzo vyake mbalimbali vya
mapato ikiwemo Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
kilichopo Dar es Salaam ambacho kinatarajiwa kukusanya mapato ya
Shilingi 3,051,000,000.00.
113. Mheshimiwa Spika,
Kituo kinategemea kukopa shilingi bilioni 2.4 kwa ajili ya miradi ya
maendeleo ya ujenzi wa jengo la maonesho na upanuzi wa Hospitali. Miradi
yote inayotekelezwa imeombewa kibali cha Msajili wa Hazina.
114. Mheshimiwa Spika, Kituo
kinaendelea kufanya taratibu za kuwezesha kujengwa kituo mahsusi cha
mikutano kitakachoitwa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mlima
Kilimanjaro. Taarifa ya upembuzi yakinifu ya mradi wa ujenzi wa Kituo
hicho iliandaliwa na Wataalamu Washauri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam. Taarifa hiyo ilionyesha kwamba mradi huo ni muhimu na wenye
manufaa kiuchumi na kijamii kwa taifa. Aidha, makadirio ya awali ya
ujenzi wa kituo hicho ni Dola za marekani milioni 248. Kwa hivi sasa
Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha kinaendelea na mazungumzo na
mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo nchini ili iweze kushiriki katika
kutekeleza mradi huo. Ni matarajio ya Wizara kuwa kuwepo kwa Kituo hicho
kutakuwa suluhisho sahihi la mahitaji ya mikutano ya kimataifa na
maonesho hapa nchini.
Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika
115. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Kujitathmini Kiutawala
Bora Barani Afrika kwa upande wa Tanzania wenye lengo la kuzisaidia nchi
za Kiafrika kuhakikisha kuwa changamoto zinageuzwa kuwa fursa za
maendeleo na mambo mazuri ya kuendelezwa kwa faida ya nchi yenyewe na
hata kuwa mfano wa kuigwa na nchi nyingine. Mpango huo unaratibiwa kwa
mujibu wa miongozo ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi za Afrika.
116. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016, Taasisi ya Mpango wa Kujitathmini
Kiutawala Bora Barani Afrika kwa upande wa Tanzania imeendelea
kutekeleza shughuli zifuatazo:-
i. Kusimamia
utekelezaji wa Mpango kazi wa kuondoa changamoto za utawala bora
zilizobainishwa kwenye ripoti ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora
Barani Afrika kwa upande wa Tanzania. Taasisi imeendelea kupokea na
kuchambua taarifa mbalimbali za utekelezaji kutoka Wizara, Idara na
Wakala wa Serikali zilizoguswa na Ripoti ya Mpango wa Kujitathmini
Kiutawala Bora Barani Afrika kwa upande wa Tanzania;
ii. Kuandaa
taarifa ya utekelezaji ya mwaka kuhusu hatua zilizochukuliwa ili
kutatua changamoto zilizojitokeza kwenye ripoti ya Mpango wa
Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika kwa upande wa Tanzania.
Taarifa hiyo inatarajiwa kuwasilishwa kwenye vikao vya Wakuu wa Nchi za
Kiafrika wanaoshiriki kwenye mchakato wa Mpango wa Kujitathmini
Kiutawala Bora Barani Afrika;
iii. Kuendelea
kutoa taarifa kwa wananchi juu ya matokeo ya tathmini ya utawala bora
kwa nchi yetu kupitia vyombo mbalimbali vya habari na majukwaa
mengineyo; na
iv. Kutafsiri
ripoti ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika kwa
upande wa Tanzania katika lugha ya Kiswahili na kuandaa chapisho la
muhtasari.
ILIYOKUWA WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
117. Mheshimiwa Spika, baada ya kuelezea utekelezaji wa majukumu ya iliyokuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
naomba sasa nilieleze Bunge lako Tukufu utekelezaji wa majukumu ya
iliyokuwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Wizara hiyo ilikuwa
na majukumu yafuatayo:-
i. Kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki zake;
ii. Kuratibu,
kushiriki na kusimamia utekelezaji wa Mtangamano wa Afrika Mashariki
hususan majadiliano na utekelezaji wa hatua za Mtangamano ambazo ni
Umoja wa Forodha; Soko la Pamoja; Umoja wa Fedha; na Shirikisho la
Kisiasa;
iii. Kutoa elimu ya Mtangamano wa Afrika Mashariki ili Wananchi waweze kuelewa na kutumia fursa za Mtangamano huo; na
iv. Kuimarisha utendaji na kujenga uwezo wa Wizara.
118. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2015/2016 Wizara hiyo iliidhinishiwa Shilingi
26,666,436,300.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi 24,047,468,300.00 ni kwa
ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi 2,618,968,000.00 ni kwa ajili
ya mishahara ya watumishi. Kiasi kilichotengwa kwa ajili ya matumizi
mengineyo kimejumuisha mchango wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki wa kiasi cha Shilingi 18,570,055,300.00.
119. Mheshimiwa Spika, hadi
kufikia tarehe 30 Aprili 2016, Wizara ilipokea jumla ya Shilingi
19,003,440,860.00, sawa na asilimia 71.26 ya fedha zote zilizotengwa.
Kati ya fedha hizo Shilingi 15,506,375,000 zilitumika kulipa
mchango wa Tanzania kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, Shilingi
1,689,936,160.00 zilitumika kulipa mishahara ya watumishi na Shilingi
1,807,129,700.00 zilitumika kutekeleza shughuli za Wizara.
120. Mheshimiwa Spika, kama
unavyofahamu Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepiga hatua
kubwa ambapo Nchi wanachama wa Jumuiya zimefikia makubaliano na
kuendelea kuyatekeleza makubaliano hayo kwenye nyanja zote za kiuchumu,
kijamii, kiutamaduni na kwa kiasi fulani kisiasa pia na hivyo kutufanya
tusilale na kutakiwa kuwa makini katika kila hatua tunazopiga.
Itakumbukwa kuwa Jumuiya yetu ilianzishwa rasmi Julai 2000 baada ya Nchi
Wanachama kukamilisha kuridhia Mkataba wa Uanzishaji wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki uliotiwa saini na Wakuu wa Nchi Wanachama tarehe 30
Novemba, 1999. Aidha, hivi sasa Nchi zote Wanachama zinatekeleza Mkataba
huu na Itifaki zake kubwa tatu (3) na zile mbalimbali za kisekta.
Maeneo yaliyobaki ambayo tunaendelea na majadiliano ni Umoja wa Fedha na
Shirikisho la Kisiasa.
121. Mheshimiwa Spika, juhudi
hizi sasa zinamaanisha kuwa eneo lote la nchi sita (6) za Jumuiya ya
Afrika Mashariki kimsingi limeungana katika nyanja mbalimbali na hivyo
kutoa motisha ya ushindani mkubwa wa ndani ya Jumuiya kiuchumi na
kimaendeleo. Kwa kutambua kuwa Tanzania ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki kupitia Wizara yangu ameelekeza Wimbo na Bendera ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki zitumike hapa nchini.
122. Mheshimiwa Spika, napenda
kuchukua nafasi hii kupitia Bunge lako Tukufu kutoa wito wa kuongezwa
kwa matumizi ya Bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye Ofisi
zote za Umma nchini zikiwemo za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na
Taasisi za Umma (tukiwemo sisi Waheshimiwa Wabunge kwenye Magari yetu na
ofisi zetu Majimboni) na zile za sekta binafsi sambamba na Bendera ya
Taifa letu Tukufu. Aidha, natoa rai kwa Taasisi za Serikali na vyombo
vya habari viweze kuutumia Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pale
ambapo Wimbo wa Taifa letu Tukufu unapigwa.
123. Mheshimiwa Spika, ni
imani yangu kuwa hatua hii itasaidia kuwajengea Watanzania uelewa,
kuifahamu vyema Jumuiya yetu na hatimae waweze kujiandaa, kushiriki na
kupata manufaa yanayoendana na fursa zilizopo kibiashara, kiuchumi,
kiuzalishaji, kijamii na kiutamaduni kwa kuzingatia uwepo wa Soko kubwa
la Afrika Mashariki na fursa zinginezo.
124. Mheshimiwa Spika, wito
huu ni moja ya utekelezaji wa Mkakati wetu wa mawasiliano wa Wizara
ambao unalenga kuwapa fursa Wananchi wetu ya kujiandaa, kuiendesha,
kuitumia Jumuiya yao na kutimiza matakwa ya Ibara ya 7(a) ya Mkataba wa
Uanzishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inasisitiza kuwa
“Jumuiya yetu hii imejengwa katika Wananchi na ushirikiano wa kimasoko”.
Aidha, hatua hizi zinalenga katika kuendeleza juhudi za Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika
kuhakikisha kuwa Jumuiya hii inakuwa kweli ni Jumuiya ya Wananchi wetu,
kutambua uwepo wake na wanufaike nayo katika kubadilisha maisha yao.
Mkutano wa 17 wa Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama na Mikutano ya 32 na 33 ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki
125. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi hiki Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa 17 wa
Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mwezi
Machi 2016 Jijini Arusha, Tanzania. Katika Mkutano huo Tanzania
iliteuliwa kwa mara ya pili mfululizo kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hadi mwezi Novemba 2016. Aidha, Mkutano
huo uliridhia Jamhuri ya Sudan Kusini kujiunga na Jumuiya ya Afrika
Mashariki ambapo tarehe 15 Aprili, 2016 nchi hiyo ilisaini Mkataba wa
Kujiunga na Jumuiya hiyo.
126. Mheshimiwa Spika, kadhalika,
katika mkutano huo Wakuu wa Nchi walizindua rasmi Pasi mpya ya
kielektroniki ya Kusafiria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuelekeza
matumizi ya hati hii mpya kuanza rasmi tarehe 1 Januari, 2017. Pasi hii
inaipandisha hadhi Pasi ya sasa ya Afrika Mashariki kutumika kusafiria
nje ya Afrika Mashariki. Nchi Wanachama zimekubaliana kuziondoa hati za
kusafiria zilizopo sasa katika kipindi cha miezi 24 kuanzia tarehe 1
Januari, 2017 hadi tarehe 31 Desemba, 2018. Hati hizo zitakuwa na alama
za jumla za kiusalama na kila Nchi Mwanachama imeruhusiwa kuongeza alama
zake za kiusalama katika Pasi hizo. Idara za Uhamiaji katika nchi
wanachama zitaendelea na jukumu la utoaji wa hati hizo kwa raia wa nchi
zao.
127. Mheshimiwa Spika, Mkutano
wa 32 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki ulifanyika
tarehe 14 Agosti, 2015 na kufikia maamuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kuidhinisha ajira kwa Mwanasheria Mkuu wa Jumuiya, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usalama wa Anga na Mkurugenzi wa Mipango katika Jumuiya.
Umoja wa Forodha
128. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa hatua ya kwanza ya Mtangamano ambayo ni Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki kama ifuatavyo:
Kanuni Mpya za Utambuzi wa Uasili wa Bidhaa
129. Mheshimiwa Spika,
katika kuziwezesha Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
kunufaika zaidi na hatua hii ya Umoja wa Forodha, mabadiliko yamefanywa
katika kanuni za utambuzi wa uasili wa bidhaa. Katika mabadiliko hayo, Nchi Wanachama zimeacha kutumia vigezo sawa kwa bidhaa zote, na sasa zitatumia vigezo tofauti kulingana na bidhaa husika. Mabadiliko haya ni
fursa kubwa kwa viwanda vya Tanzania ambavyo vingi bado ni vidogo na
vilikuwa haviwezi kufikia vigezo vya uasili wa bidhaa. Aidha, katika
kipindi hiki, nchi Wanachama wa Jumuiya zilikamilisha mwongozo wa
kutumika katika kurahisisha utekelezaji wa kanuni hizo.
Uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Kiforodha
130. Mheshimiwa Spika, katika
kuweka mazingira wezeshi ya biashara katika Jumuiya, Wizara imeendelea
kuratibu uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Kiforodha kupitia Kamati ya
Kitaifa na Kikanda ya uondoaji wa vikwazo hivyo. Katika mwaka wa fedha
2015/2016 vikwazo 16 viliripotiwa vimeondolewa, kati ya hivyo vinne (4)
viliihusu Tanzania. Vikwazo hivyo ni tozo ya Dola za Marekani 200 kwa
kila kontena la kemikali; kutopewa upendeleo wa ushuru wa forodha kwa
chumvi na bidhaa za plastiki kutoka Kenya; na upimaji wa malori matupu.
131. Mheshimiwa Spika,
ili kuharakisha uondoaji wa vikwazo visivyo vya kiforodha, Wizara
imekuwa na utaratibu wa kuitisha mikutano ya pande mbili husika. Katika
kipindi hiki Wizara ilifanya mikutano na Kenya na Burundi ambayo
ilichangia kuharakisha uondoaji wa vikwazo visivyo vya kiforodha
vikiwemo vile vilivyotajwa hapo juu. Vilevile, tumekubaliana na Kenya
kufanya utafiti juu ya tozo zinazotozwa na mamlaka za Serikali za mitaa
za nchi zetu zinazoathiri biashara baina yetu kwa lengo la kurazinisha
tozo hizo.
Mwenendo wa Biashara ya Bidhaa kati ya Tanzania na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
132. Mheshimiwa Spika, nafasi
ya Tanzania katika Soko la Jumuiya imeendelea kupanda kutoka asilimia
18 mwaka 2010 hadi asilimia 26 mwaka 2014 na tunategemea kufanya vizuri
zaidi kutokana na juhudi zinazoendelea za kudhibiti ulanguzi wa mazao na
bidhaa mipakani, utekelezaji wa sheria mpya ya uasili wa bidhaa,
kuondoa vikwazo visivyo vya kiforodha na kuimarisha uzalishaji
viwandani. Kwa mujibu wa Taarifa ya Biashara ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya mwaka 2014, biashara ndani ya Jumuiya imekua na kufikia
Dola za Marekani bilioni 5.63 kwa mwaka 2014 ikilinganishwa na Dola za
Marekani bilioni 3.72 kwa mwaka 2010. Aidha, biashara baina ya Tanzania
na Nchi Wanachama imeendelea kuimarika na kuongezeka kutoka Dola za
Marekani bilioni 0.69 mwaka 2010 na kufikia Dola za Marekani bilioni
1.49 mwaka 2014. Kwa mwaka 2013 kiwango cha biashara kiliongezeka zaidi
kulingana na hali ya mahitaji ya soko na kupanda kwa uzalishaji kwenye
sekta mbalimbali. Tanzania imeendelea kuwa na urari chanya wa biashara
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kama inavyoonekana katika Kiambatisho Na. 1.
133. Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara wa Tanzania wamendelea kuchangamkia fursa zitokanazo na Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki.Wafanyabiashara hao wamefanikiwa kuuza
kwa wingi katika Soko la Afrika Mashariki bidhaa za viwandani kama vile
transfoma, waya za umeme, vyandarua, saruji na magunia; na bidhaa za
kilimo kama vile mahindi, mchele, katani, mbogamboga, asali na chakula
cha mifugo. Hii inaashiria kuendelea kuimarika kwa biashara ya bidhaa za
viwandani na mazao ya kilimo.
134. Mheshimiwa Spika, bidhaa zilizonunuliwa kwa wingi kutoka Nchi Wanachama ni pamoja na kemikali kwa ajili ya viwanda vya nguo, vipodozi na sabuni; dawa
za binadamu na mifugo; vipuri vya magari; vifuniko vya chupa za
vinywaji; sabuni; vifaa vya kufanyia usafi; vifungashio; mabanda maalum
ya kilimo cha mbogamboga na maua (green house); na vyumba vya baridi kwa
ajili ya kuhifadhia bidhaa mbalimbali.
Umoja wa Fedha
135. Mheshimiwa Spika, Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeendelea kutekeleza Mpangokazi wa Miaka
Kumi wa Kuelekea katika Eneo la Sarafu Moja ulioanza kutekelezwa mwaka
2014 na utakaokamilika mwaka 2024. Katika kutekeleza Mpangokazi huo,
Nchi Wanachama zimekamilisha majadiliano
ya Muswada wa Sheria ya uanzishwaji wa Taasisi ya Fedha ya Afrika
Mashariki na Taasisi ya Takwimu ya Afrika Mashariki. Maandalizi ya
majadiliano ya muswada wa Kamisheni ya Ufuatiliaji na Usimamizi ya
Afrika Mashariki yataanza katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha.
136. Mheshimiwa Spika, matarajio
ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuifikia hatua hii
muhimu ya kuanzisha matumizi ya sarafu moja kwenye eneo la Jumuiya
ifikapo mwaka 2024. Hatua hii itafikiwa mara baada ya Nchi Wanachama
angalau watatu (3) kufikia vigezo vya kiuchumi vilivyoainishwa kwenye
Itifaki ya Umoja wa Fedha. Aidha, hatua hiyo itatanguliwa na uanzishwaji
wa Benki Kuu ya Afrika Mashariki ambayo pamoja na majukumu mengine
itakuwa na majukumu ya kuchapisha na kusambaza sarafu hiyo ya Afrika
Mashariki.
Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki
137. Mheshimiwa Spika, Shirikisho
la Kisiasa ni hatua ya nne na ya mwisho katika mtangamano wa Afrika
Mashariki ambayo inategemea sana misingi imara itokanayo na utekelezaji
wa hatua za mwanzo za mtangamano. Katika kipindi cha mwaka fedha
2015/2016, Nchi Wanachama ziliendelea na majadiliano ya modeli ya
shirikisho ambayo itatumika katika kuandaa Rasimu ya Katiba ya
Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki.
138. Mheshimiwa Spika, rasimu
hiyo, inatarajiwa kutumika katika kuelimisha na kuhamasisha wananchi wa
Afrika Mashariki kuhusu aina ya Shirikisho linalotarajiwa kuundwa ili
kuleta uelewa wa pamoja na uungwaji mkono wa hatua hiyo wakati ukifika.
Aidha, kwa kuwa Shirikisho la Kisiasa ni mchakato, Nchi Wanachama
zimeendelea na utekelezaji wa shughuli zinazounda msingi wa Shirikisho
hilo ikiwemo masuala ya utawala bora, uimarishaji wa demokrasia na
utawala wa sheria.
Ushirikiano na Kanda nyingine za Kiuchumi
Majadiliano
ya Kuanzisha Eneo Huru la Biashara la Utatu wa Soko la Pamoja la
Mashariki na Kusini mwa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya
ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
139. Mheshimiwa Spika, juhudi
za kuziunganisha Jumuiya za COMESA, EAC na SADC ili kuwa eneo moja huru
la kibiashara zimefika hatua nzuri. Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi za
COMESA, EAC na SADC uliofanyika tarehe 10 Juni, 2015 Jijini Sharm El
Sheikh, Misri ulihitimishwa kwa Wakuu wa Nchi na Serikali kutia saini
Azimio la Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara; na Mkataba wa
Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara.
140. Mheshimiwa Spika, kufuatia
kusainiwa kwa mkataba huo, Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya
hizo walikubaliana kukamilisha majadiliano ya maeneo yaliyosalia katika
kipindi cha miezi 6 hadi 12 baada ya uzinduzi rasmi wa eneo huru la
biashara. Maeneo hayo ni uondoshwaji wa kodi kwenye bidhaa, utambuzi wa
uasili wa bidhaa, usuluhishi wa migogoro ya kibiashara na kupunguziana
ushuru.
Majadiliano ya Uhuru wa Wafanyabiashara kusafiri katika Eneo la Utatu
141. Mheshimiwa Spika, ili
kurahisisha na kuwezesha wafanyabiashara kusafiri katika Eneo hilo la
Utatu, Nchi Wanachama zimeendelea na majadiliano ya kuandaa Mkataba wa
Uhuru wa Wafanyabiashara kusafiri kwenye eneo hilo. Mkataba huo unatarajiwa kuidhinishwa ifikapo Desemba, 2016.
Majadiliano ya Uendelezaji wa Viwanda katika Eneo la Utatu
142. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu ushiriki wa Tanzania katika kukamilisha Rasimu ya Mpango wa
Maeneo ya Ushirikiano katika Maendeleo ya Viwanda; na Mpangokazi kwa
ajili ya Utekelezaji wa utaratibu wa Ushirikiano katika eneo la Utatu. Maeneo
yaliyoboreshwa ni Sera na Mikakati kutoka Kanda zote tatu; Uzingatiaji
wa uendelezaji wa viwanda unaojali utunzaji wa mazingira; na Utambuaji
Kisheria na Umiliki wa Haki zinazotokana na Uvumbuzi na Ubunifu katika
maendeleo ya Viwanda. Aidha,
Nchi Wanachama zimekubaliana kushirikiana katika maeneo ya uratibu na
uhamasishaji wa pamoja wa sera ya maendeleo ya viwanda na uongezaji
thamani bidhaa baina ya nchi Wanachama; na Uendelezaji wa Viwanda Vidogo
na vya Kati na kujenga uwezo wa utaalam katika kuendeleza Viwanda.
Ubia wa Kiuchumi kati ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya
143. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu majadiliano ya Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi baina ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya. Malengo
ya ubia huu ni kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuleta maendeleo
endelevu na kuziwezesha nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki kupata
misaada ya kimaendeleo ili kukabiliana na changamoto za uzalishaji na
kuweka muda wa kuondoa vikwazo vya biashara.
144. Mheshimiwa Spika, nchi
za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya zilikamilisha mapitio
ya kisheria ya Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi baina ya nchi hizo. Hatua
inayoendelea ni Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutafsiri mkataba
huo katika lugha ya Kiswahili wakati Umoja wa Ulaya unatafsiri mkataba
huo katika lugha 21 zinazotumiwa na Jumuiya ya Ulaya. Baada ya
kukamilika kwa mchakato wa kufanya tafsiri, Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya zitasaini Mkataba huo, pamoja na
kuuridhia ili utekelezaji wake uanze.
145. Mheshimiwa Spika, ili
kuweka mazingira wezeshi ya kukuza na kuendeleza viwanda vya nguo na
ngozi ndani ya Jumuiya, Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi Wanachama
ulielekeza Nchi Wanachama kuhakikisha zinapunguza uingizaji wa nguo na
viatu vilivyotumika kutoka nje ya Jumuiya na kusitisha uagizaji wake
katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu wa fedha. Aidha,
Wakuu wa Nchi walielekeza Nchi wanachama kupiga marufuku utaratibu wa
kuuza ngozi na bidhaa za ngozi ghafi nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kujengea uwezo na upatikanaji wa masoko kwa Wajasiriamali wadogo
146. Mheshimiwa Spika, Maonesho
ya 16 ya Juakali/Nguvukazi yaliyofanyika tarehe 30 Novemba hadi 6
Disemba 2015 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es
Salaam katika maonesho hayo jumla ya wajasiriamali 734 kutoka Nchi
zote wanachama walishiriki. Kati ya hao, wajasiriamali 395 walikuwa ni
washiriki kutoka Tanzania. Lengo la maonesho hayo ni kujenga uwezo wa
wafanyabiashara wadogo kupata masoko ya bidhaa zao katika Nchi
Wanachama. Napenda kutoa rai kwa wajasiriamali wa Tanzania kushiriki
katika Maonesho ya 17 ya Juakali/Nguvukazi yaliyopangwa kufanyika mwezi
Novemba 2016 nchini Kenya.
Uendelezaji wa Miundombinu ya Kiuchumi
147. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kuratibu utekelezaji wa programu na miradi ya kitaifa yenye
sura ya Kikanda iliyoainishwa katika Mipango ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya Uendelezaji wa Miundombinu ya Kiuchumi. Hatua zilizofikiwa
katika uendelezaji wa programu na miradi hiyo ni kama ifuatavyo:
Ujenzi wa Vituo vya Kutoa Huduma kwa Pamoja Mipakani
148. Mheshimiwa Spika,
Wizara imeendelea kuratibu ujenzi wa vituo vya kutoa huduma kwa pamoja
mipakani. Hadi sasa vituo viwili (2) kati ya saba (7) vinavyojengwa kwa
uratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki vimekamilika na kuzinduliwa.
Vituo hivyo ni kituo cha Holili/Taveta mpakani mwa Tanzania na Kenya; na
kituo cha Rusumo mpakani mwa Tanzania na Rwanda.
149. Mheshimiwa Spika,
vilevile, Wizara iliratibu ukamilishaji wa Kanuni za Utekelezaji wa
Sheria ya Jumuiya ya Kusimamia Uendeshaji wa Vituo vya Kutoa Huduma kwa
Pamoja Mipakani. Kanuni hizo zimepitishwa na Mkutano wa 33 wa Baraza la
Mawaziri la Jumuiya uliofanyika mwezi Februari, 2016. Ili kupata uelewa wa pamoja kuhusu Vituo vya Kutoa Huduma kwa Pamoja Mipakani, Wizara
iliratibu na kushiriki katika mafunzo kwa maafisa wa Serikali, sekta
binafsi na wawakilishi wa jamii kwa Vituo vya Horohoro na Sirari.
Taarifa kuhusu vituo vingine na hatua zilizofikiwa ili kuwezesha kuanza
kutoa huduma stahiki ni kama inavyoonesha katika Kiambatisho Na. 2.
150. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu ukamilishaji wa ujenzi wa Daraja la Kimataifa la Rusumo ikiwa ni sehemu ya kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuimarisha vituo vya kutoa huduma za pamoja mipakani katika ushoroba wa kati. Daraja hilo lenye uwezo wa kupitisha magari manne kwa wakati mmoja yenye uzito wa tani 56 kila mojalilizinduliwa rasmi na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Paul Kagame, Rais wa Jamhuri ya Rwanda tarehe 6 Aprili, 2016.
Uendelezaji wa Mtandao wa Barabara
151. Mheshimiwa Spika, hatua zilizofikiwa katika uendelezaji wa mtandao wa barabara za Kikanda katika mwaka 2015/2016 ni kama ifuatavyo:
Mradi wa Barabara ya Arusha – Holili/Taveta – Voi
152. Mheshimiwa Spika, mradi huu unahusu uendelezaji wa mtandao wa barabara unaoziunganisha nchi
za Tanzania na Kenya kupitia mpaka wa Holili/Taveta yenye urefu wa
kilomita 234.3. Kwa upande wa Tanzania, awamu ya kwanza ya ujenzi wa
barabara hiyo kwa kiwango cha lami unahusisha upanuzi wa sehemu ya
kutoka Arusha hadi Tengeru yenye urefu wa kilometa 14.1 kuwa njia nne na
barabara ya mzunguko wa kusini mwa Jiji la Arusha yenye urefu wa
kilometa 42.41. Aidha, kwa upande wa Kenya mradi unahusisha ujenzi wa
barabara mpya ya lami yenye urefu wa kilomita 100 kutoka Taveta hadi
Mwatate. Gharama za mradi kwa upande wa Tanzania ni
takriban Shilingi bilioni 209.61 ambapo kati ya hizo Benki ya Maendeleo
ya Afrika itatoa Shilingi bilioni 190.21 na Serikali ya Tanzania itatoa
Shilingi bilioni 19.4.
153. Mheshimiwa Spika, Jiwe
la Msingi la Ujenzi wa Barabara hiyo liliwekwa mwezi Machi, 2016 na
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Mheshimiwa Uhuru MuigaiKenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya.
Uwianishaji wa Uzito wa Magari Katika Barabara
154. Mheshimiwa Spika, Sheria
ya Udhibiti wa Uzito wa Magari ya Mwaka 2013 iliyopitishwa na Bunge la
Afrika Mashariki imeridhiwa na Nchi zote Wanachama. Nchi Wanachama
zimekamilisha majadiliano ya kuandaa Kanuni za kuwezesha utekelezaji wa
Sheria hizo ambazo zilipitishwa katika Mkutano wa 33 wa Baraza la
Mawaziri la Jumuiya uliofanyika Jijini Arusha mwezi Februari, 2016.
Mkakati wa Kuwezesha Sekta ya Uchukuzi
155. Mheshimiwa Spika, Nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeidhinisha utekelezaji wa
Mkakati wa Kuwezesha Sekta ya Uchukuzi. Mkakati huo unazitaka Nchi
Wanachama pamoja na masuala mengine kuwianisha mitaala ya mafunzo ya
udereva wa magari ya biashara; usajili wa vyombo vya moto; na madaraja
ya leseni. Nchi Wanachama zimekamilisha rasimu za mitaala ya mafunzo ya
udereva wa magari ya biashara.
Sekta ya Mawasiliano
156. Mheshimiwa Spika, Wizara
inaendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Kutatua Changamoto ya
Gharama Kubwa za Maunganisho ya Simu za Mkononi katika Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki kama ulivyoridhiwa na Wakuu wa Nchi wa
Jumuiya hiyo mwezi Februari, 2015. Katika kutekeleza mpango huo,
yamefanyika mapitio
ya Kanuni zinazotumika katika mfumo wa kuongoza sekta ya mawasiliano
nchini. Wizara ya kisekta inafanya tathmini ya changamoto zilizoibuliwa
na wadau kuhusu mpango huo.
Sekta ya Hali ya Hewa
157. Mheshimiwa Spika, Itifaki
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Ushirikiano katika Huduma za Hali ya
Hewa ilisainiwa na Mawaziri wanaosimamia masuala ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki kutoka Nchi Wanachama katika Mkutano wa 33 wa Baraza la
Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mwezi Februari,
2016. Itifaki hiyo inatoa mwongozo wa ushirikiano wa Nchi Wanachama
katika kubadilishana taarifa na ujuzi katika masuala ya hali ya hewa. Nchi Wanachama zimekubaliana kuridhia Itifaki hiyo kabla ya mwezi Julai, 2016.
Sekta ya Bandari na Usafiri Majini
158. Mheshimiwa Spika, katika
jitihada za kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki, Nchi Wanachama zinaendelea na maandalizi ya Mkakati
wa Usafiri wa Majini wa Afrika Mashariki. Katika kutekeleza azma
hiyo, Utafiti
wa Awali wa Hali ya Usafiri wa Majini na Sekta ya Bandari umekamilika.
Ripoti ya Utafiti huo, pamoja na mambo mengine, imebainisha changamoto
katika utekelezaji wa miradi ya kuendeleza Bandari katika mwambao wa
Bahari ya Hindi, Maziwa na Uanzishaji wa Bandari Kavu. Changamoto hizo
ni pamoja na uhaba wa rasilimali fedha zinazohitajika katika kutekeleza
Miradi iliyoainishwa katika Mipango Mikuu ya kuendeleza Bandari za Nchi
Wanachama na haja ya kuwianisha Mifumo ya Kitaasisi na Udhibiti katika
Sekta ya Usafiri wa Majini miongoni mwa Nchi Wanachama ili kuwa na
viwango vinavyofanana katika udhibiti wa vyombo vya majini. Maoni ya Ripoti hiyo yatasaidia katikamaandalizi ya Mkakati wa Afrika Mashariki wa Usafiri wa Majini.
Sekta ya Nishati
159. Mheshimiwa Spika, wakati
wa Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki uliofanyika mwezi Machi 2016, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Uganda walifanya Kikao cha pamoja
kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda mpaka bandari ya Tanga litakalokuwa na urefu wa kilometa 1,410.
160. Mheshimiwa Spika, kufuatia Kikao
hicho cha Marais wawili, wataalam wa pande zote mbili waliendelea na
majadiliano yaliyopelekea Serikali ya Uganda kutoa tamko rasmi kwenye Mkutano
wa 13 wa Ushoroba wa Kaskazini uliofanyika mwezi Aprili, 2016 Jijini
Kampala kuwa bomba hilo litajengwa kupitia Tanzania. Mradi huo
utagharimu Dola za Marekani bilioni nne na kukamilika baada ya miaka
mitatu hadi minne. Mradi huo unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa
moja takriban 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000. Aidha,
Benki ya Maendeleo ya Afrika imeidhinisha msaada wa kiasi cha Dola za
Marekani 1,691,130 kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Mradi
mwingine wa Bomba la Mafuta la Mbarara - Mwanza - Isaka - Dar es
Salaam. Fedha za nyongeza Dola za Marekani 95,600 zinahitajika ili
kukamilisha upembuzi yakinifu huo. Hivyo, kila Nchi Mwanachama imetakiwa
kuchangia kiasi cha Dola za Marekani 19,120 kabla ya mwisho wa mwezi
Juni, 2016 ili kukamilisha upembuzi yakinifu wa Mradi huo.
Ushirikiano Katika Sekta za Huduma za Jamii
Sekta ya Elimu, Utamaduni na Michezo
Urazinishaji wa Mitaala
161. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na uratibu wa zoezi laurazinishaji wa Mitaala kwa ngazi zote za Elimu pamoja na mafunzo ya ualimu kwa shule za awali, msingi na sekondari.
Shindano la Insha la Jumuiya
162. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania katika shindano la uandishi wa Insha la Jumuiya
ya Afrika Mashariki lililoshirikisha wanafunzi wa shule za sekondari
kutoka nchi tano (5) Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nafurahi
kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa kijana Mtanzania Simon
Mollel Sabaya kutoka Shule ya Sekondari ya Mzumbe aliibuka mshindi wa
kwanza katika shindano hilo. Huu ni ushahidi kuwa vijana wetu wanaweza na wanauelewa wa Jumuiya yetu.
Naomba nitumie fursa hii kutoa pongezi kwa kijana huyu na kuwatia moyo
vijana wengine waendelee kushiriki kwenye mashindano haya ili waweze
kuliletea sifa Taifa letu. Natoa wito kwa walimu na wazazi
kuwahamasisha wanafunzi kushiriki katika shindano hilo ili kukuza uelewa
wao katika masuala ya Jumuiya.Wizara
yangu kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki; Wizara za Elimu,
Sayansi na Teknolojia; na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
itaanzisha kampeni ya kuongeza uelewa wa Jumuiya katika shule na vyuo.
Mdahalo wa Nne wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu
163. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu ushiriki wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Tanzania katika
mdahalo wa Nne (4) wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki uliofanyika mwezi Desemba 2015, Kampala, Uganda. Lengo
la mdahalo huo ni kupata washindi wawili kutoka kila Nchi Mwanachama wa
Jumuiya ambao watakuwa Mabalozi wa Nchi zao katika masuala ya Jumuiya.
Kwa upande wa Tanzania, washindi wa mwaka 2015 ni Raphael Kambamwene wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Lucy Peter Funja wa Chuo Kikuu cha
Ardhi. Aidha, Wizara inaendelea na jukumu la kuwapatia taarifa Mabalozi
hao zitakazowawezesha kutoa elimu kwa umma hususan kwa vijana wenzao.
Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki
164. Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba Kamisheni ya Kiswahili
ya Afrika Mashariki imeshahamia rasmi katika Makao Makuu yake yaliyopo
Zanzibar. Hii ni kufuatia kusainiwa kwa Mkataba wa Uenyeji baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tarehe 28 Desemba, 2015.
Mradi wa Hifadhi ya Mazingira Katika Bonde la Ziwa Victoria Awamu ya Pili
165. Mheshimiwa Spika, katika
kukabiliana na athari za mazingira zinazotokana na shughuli za binadamu
katika Bonde la Ziwa Victoria zilizosababisha pamoja na mambo mengine
kupungua kwa kina cha maji na samaki katika ziwa, Wizara imeendelea na uratibu wa utekelezaji
wa shughuli za Mradi wa Usimamizi wa Mazingira katika Bonde la Ziwa
Victoria. Katika kipindi hiki, Benki ya Dunia iliongeza muda wa miaka
miwili na nusu kuanzia mwezi Juni 2015 hadi mwezi Desemba 2017 na mkopo
wa Dola za Marekani milioni 10 ambazo zitatumika kukamilisha miradi
ambayo ilikuwa haijakamilika katika Awamu ya Pili ya Mradi iliyofikia
ukomo wake mwezi Juni 2015 na kuandaa Awamu ya Tatu. Vilevile, udhibiti wa magugumaji katika Ziwa Victoria umeendelea ambapo magugumaji yamepungua
Ziwani kutoka hekta 520 mwezi Septemba, 2009 hadi hekta 104 mwezi
Novemba, 2015. Mradi umeendelea na shughuli za udhibiti wa utupaji taka
na uhamasishaji wa uzalishaji bora viwandani ambapo Jumla ya viwanda 118
sawa na asilimia 86 vimepata mafunzo ya uzalishaji bora viwandani.
Programu ya Hifadhi ya Mazingira kwa Kuboresha Sera, Mabadiliko ya Tabianchi, Utafiti na Maendeleo ya Kiuchumi
166. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kunakuwa na matumizi endelevu ya rasilimali maji katika Bonde la Mto Mara, Wizara
yangu imefanikisha utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya Usimamizi wa
pamoja wa rasilimali maji katika Bonde la Mto Mara kati ya Tanzania na
Kenya. Makubaliano hayo yatasaidia kupunguza athari za mazingira
zinazosababishwa na shughuli za binadamu katika bonde hilo.
Mradi wa Idadi ya Watu, Afya na Mazingira wa Jumuiya
167. Mheshimiwa Spika, ili
kujenga uelewa wa pamoja kwa wananchi katika masuala ya idadi ya watu,
afya na mazingira kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu, Wizara
imeendelea kuratibu ushiriki wa Tanzania katika maandalizi ya Mpango
Mkakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Masuala ya Idadi
ya Watu, Afya na Mazingira. Mpango huo utakapokamilika utatoa mwongozo
wa kuzingatia masuala ya idadi ya watu, afya na mazingira katika
utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Nchi Wanachama.
Sekta ya Jinsia na Maendeleo ya Jamii
168. Mheshimiwa Spika, nafasi ya wanawake, watoto na vijana imeendelea kupewa kipaumbele katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa muktadha huo, Wizara
imeendelea kuratibu programu na miradi inayolenga kuyajengea uwezo
makundi hayo ili kunufaika na fursa mbalimbali zinatokanazo na
Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, progamu hizi zimetoa
fursa kwa makundi hayo kutoa maoni yao ya namna bora ya kuendeleza
mtangamano. Vilevile, Jumuiya ya Afrika Mashariki inakamilisha Sera ya Watoto ya Jumuiya.
Ushirikiano katika Siasa, Ulinzi na Usalama
169. Mheshimiwa Spika, naomba
kuchukua nafasi hii kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa Jumuiya ya
Afrika Mashariki imepata Katibu Mkuu mpya Balozi Liberat Mfumukeko
kutoka Jamhuri ya Burundi atakeyeiongoza Jumuiya kwa Kipindi cha miaka
mitano ijayo. Aidha, naomba kumshukuru Balozi Dkt. Richard Sezibera
kutoka Jamhuri ya Rwanda kwa mchango wake mkubwa katika kuiendesha
Jumuiya kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Ushirikiano katika Siasa
170. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki tumeendelea kushuhudia kushamiri kwa demokrasia katika Nchi Wanachama wa Jumuiya. Kwa kuzingatia kwamba demokrasia ni moja ya misingi mikuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wizara yangu imeendelea kuratibu ushiriki wa Tanzania katika timu ya waangalizi wa uchaguzi mkuu kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki kushiriki katika uangalizi wa uchaguzi mkuu katika Nchi
Wanachama. Katika kipindi hiki, Nchi tatu Wanachama wa Jumuiya
zilifanya uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge. Nchi hizo ni Jamhuri ya
Burundi, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uganda. Jamhuri
ya Burundi ilifanya Uchaguzi wake mwezi Julai, 2015 ambapo Rais Pierre
Nkurunziza aliibuka mshindi wa Uchaguzi huo. Aidha, kwa upande wa
Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, Wizara iliratibu ushiriki wa waangalizi wa
uchaguzi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki waliokuja kufanya uangalizi
ambapo Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipata ushindi katika uchaguzi huo.
171. Mheshimiwa Spika, Wizara
pia iliratibu ushiriki wa Tanzania katika timu ya waangalizi wa
uchaguzi wa Jumuiya kwenye uchaguzi mkuu wa Uganda uliofanyika mwezi
Februari, 2016. Katika uchaguzi huo, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, Rais
Mstaafu wa Awamu ya Pili alipewa heshima ya kuwa Kiongozi wa timu hiyo
kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Mheshimiwa Rais Yoweri Kaguta
Museveni aliibuka mshindi.
172. Mheshimiwa Spika, katika kuwashirikisha zaidi wananchi wa Afrika Mashariki kuchangia maoni yao katika maamuzi mbalimbali ya uendeshaji wa Jumuiya, Wizara
yangu iliwawezesha Wananchi wa Tanzania kupitia asasi zao kushiriki
katika Mkutano wa Katibu Mkuu wa Jumuiya na Asasi Zisizo za Kiserikali
na Sekta Binafsi uliofanyika mwezi Machi, 2016 Dar es Salaam, Tanzania.
Maazimio ya Mkutano huo yalikuwa ni pamoja na kuliomba Baraza la
Mawaziri la Jumuiya kuharakisha matumizi ya vituo vya utoaji wa huduma
kwa pamoja mipakani, utekelezaji wa himaya moja ya forodha; na
kushirikisha sekta binafsi katika ngazi zote za mchakato wa uchaguzi ili
kuweka mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao.
Bunge la Afrika Mashariki
173. Mheshimiwa spika, Wizara
iliratibu na kushiriki katika mikutano ya Bunge la Afrika Mashariki,
ambapo Bunge hilo lilijadili na kupitisha Miswada ya Sheria za Jumuiya,
Maazimio na Taarifa mbalimbali. Miswada iliyopitishwa ni pamoja na
Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Kupunguza na
Kukabiliana na Majanga wa mwaka 2012;Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Miamala ya Kielektroniki wa mwaka 2014; Muswada
wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Tasnia ya Ubunifu na
Utamaduni wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka 2015; na Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Usimamizi na Uhifadhi wa Misitu wa mwaka 2015.
174. Mheshimiwa spika, aidha, Miswada iliyosomwa Bungeni kwa mara ya kwanza ni: Muswada
wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Usawa wa Jinsia na
Maendeleo wa mwaka 2016; Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya Kulinda Watoa Taarifa wa mwaka 2016; Muswada wa Sheria ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Mafao ya Kustaafu kwa baadhi ya Wakuu wa
Taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka 2016; Muswada
wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Marekebisho ya Sheria ya
Usimamizi wa Forodha ya Afrika Mashariki wa mwaka 2016; naMuswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu wa mwaka 2016.
175. Mheshimiwa spika, Vilevile, Bunge
lilitoa Maazimio kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kusisitiza Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika ya kuanzisha Bunge la
Afrika; Kuridhia Itifaki ya Sheria ya Ushauri ya Umoja wa Afrika inayohusiana na Bunge la Afrika; Kumpongeza
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushindi wake katika uchaguzi Mkuu
pamoja na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kudumisha
Amani na Demokrasia wakati wa Uchaguzi; Azimio
la Bunge la Kuzitaka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
kuchukua hatua za haraka katika kudhibiti Usafirishaji haramu wa
binadamu; na Azimio la Bunge la kuwashukuru Wake wa Viongozi wa Nchi Waanzilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
176. Mheshimiwa spika, Kamati
ya Bunge la Afrika Mashariki ya Masuala ya Kikanda na Utatuzi wa
Migogoro ilifanya ziara ya Uangalizi na tathmini ya changamoto za
utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja katika Kanda ya Kati mwezi
Novemba 2015. Kamati hiyo na Uongozi wa Wizara ilijadili hali halisi ya
utekelezaji wa makubaliano ya Itifaki hiyo hususan katika kanda ya kati
ambapo kati ya masuala yaliyoibuliwa ni kuhusu afya ya Wananchi katika
kutumia uhuru wa watu wa Jumuiya kuingia na kutoka Nchi za Jumuiya
ambapo walisisitiza kuhusu umuhimu wa Chanjo ya Homa ya Manjano ili
kuzuia uambukizaji wa ugonjwa huo.
177. Mheshimiwa Spika, Kamati
mbalimbali za Bunge la Afrika Mashariki zilifanya mikutano ya kukusanya
maoni ya wadau kuhusu utungwaji wa sheria mbalimbali za Jumuiya ambapo
Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji ilikusanya maoni ya
Muswada wa Sheria ya Sectional Properties Bill, 2016, Kamati ya Kilimo, Maliasili na Mazingira ilikusanya maoni kuhusu Muswada wa Sheria ya Usimamizi na Uhifadhi wa Misitu wa Afrika Mashariki wa mwaka 2015 na Kamati ya General Purpose ilikusanyamaoni kuhusu Muswada wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2015.
178. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu Programu ya Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Jumuiya ya
kutoa elimu kwa umma iliyohusisha Vyombo vya Habari, Taasisi za Elimu,
Asasi za Kiraia, Wabunge na Maafisa wa Serikali mwezi Aprili, 2016.
Lengo la programu hiyo pamoja na mambo mengine ni kuhamasisha umma juu
ya fursa zitokanazo na Jumuiya ili kunufaika nazo.
Ushirikiano katika Ulinzi
179. Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha
uwezo wa vyombo vya ulinzi na usalama vya Nchi Wanachama katika
urejeshaji amani wakati wa machafuko, kukabiliana na ugaidi, uharamia na
majanga, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania katika zoezi la kijeshi
kwa vyombo vya ulinzi na usalama kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki la Vituo vya Kamandi lijulikanalo kama ‘Ushirikiano Imara 2016’. Zoezi hilo lilifanyika mwezi Machi 2016 nchini Kenya.
Ushirikiano katika Usalama
180. Mheshimiwa Spika, kwa
kuzingatia kuwa amani na usalama ni nguzo kuu kwa maendeleo ya kijamii
na uchumi katika Jumuiya, Wizara yangu iliratibu ushiriki wa Tanzania
katika mkutano wa Wakuu wa Upelelezi toka Jeshi la Polisi, Wasajili wa
Magari, Wakuu wa Kupambana na Madawa ya Kulevya na Wakuu wa Vitengo vya
Kupambana na Biashara Haramu ya Watu uliofanyika mwezi Desemba 2015
Nairobi, Kenya. Mkutano huo ulitoa fursa kwa wakuu hao kubadilishana
uzoefu na taarifa za mienendo ya uhalifu katika maeneo yao na kupanga
mpango wa pamoja wa operesheni za kupambana na uhalifu. Aidha, Nchi
Wanachama zinaendelea kutekeleza Mkakati wa Kikanda wa Amani na Usalama.
181. Mheshimiwa Spika,
napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Jamhuri ya Sudan Kusini
imejiunga rasmi na Jumuiya na hivyo kuifanya idadi ya Nchi Wanachama
kuongezeka kutoka tano hadi sita. Nchi ya Sudan Kusini, iliwasilisha
rasmi maombi ya kujiunga na Jumuiya mwezi Novemba, 2011. Nchi Wanachama
zilikamilisha mchakato wa uhakiki kuthibitisha iwapo nchi hiyo inakidhi
vigezo kulingana na matakwa ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi Wanachama uliofanyika
mwezi Machi 2016 jijini Arusha uliridhia nchi hiyo kujiunga na Jumuiya.
182. Mheshimiwa Spika, Wakuu
wa Nchi wanachama wa Jumuiya walimpa heshima Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa
Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya kusaini Mkataba wa Jamhuri
ya Sudan Kusini kujiunga na Jumuiya kwa niaba yao. Zoezi la utiaji
saini Mkataba huo, lilifanyika Dar es Salaam tarehe 15 Aprili, 2016.
183. Mheshimiwa Spika, kujiunga
kwa Jamhuri ya Sudan Kusini kumeifanya Jumuiya kuwa na jumla ya watu
zaidi ya milioni 160, hii ni fursa ya kipekee kwa sekta binafsi hapa
nchini katika kuendeleza na kukuza biashara zao. Naomba kuchukua nafasi
hii kuishauri sekta binafsi hapa nchini kuchangamkia fursa zitokanazo na
kupanuka kwa soko la Jumuiya.
184. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kutekeleza Mkakati wake wa Mawasiliano kwa kutoa Elimu kwa
Umma kuhusu fursa zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na jinsi
ya kunufaika nazo. Wizara ilitumiamaonesho
mbalimbali kama vile ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Saba Saba, Nane Nane,
Maonesho ya Biashara Zanzibar, maonesho ya Siku ya Mara, Maonesho ya
Siku ya Wafanyakazi Duniani na Juakali/Nguvu Kazi ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki kutoa elimu kwa Umma. Jumla ya nakala za machapisho 11,046 yenye taarifa muhimu na fursa zipatikanazo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki yalisambazwa
na jumla ya wananchi 7,387 walitembelea Mabanda ya Wizara ili kupata
taarifa na ufafanuzi wa masuala ya mtangamano. Taarifa za maonesho hayo
zilisambazwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo Luninga,
tovuti na blogu ya Wizara. Vilevile, makala ya Televisheni yenye ujumbe
wa fursa mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki ilioneshwa katika
Luninga za TBC1, Star TV, Channel 10 naClouds TV.
185. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu iliweka mabango saba katika
mipaka ya Namanga, Horohoro, Holili, Sirari, Mutukula, Rusumo na
Kabanga yenye kuelezea taratibu za kufuatwa na wafanyabiashara wakati wa
kuuza na kununua bidhaa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
186. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliendesha mikutano ya elimu kwa umma katika Mikoa ya Mwanza,
Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Mara, Kagera, Mtwara, Lindi na katika mipaka
ya Mutukula, Rusumo, Kabanga, Holili na Namanga. Aidha, Wizara
iliendesha warsha ya Waandishi wa Habari wa Zanzibar kwa lengo la
kuwaelimisha juu ya fursa na masuala ya Mtangamano ili waweze kufikisha
taarifa sahihi za Mtangamano kwa wananchi.
187. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliendelea kuimarisha uwezo wa kiutendaji kwa kupandisha vyeo watumishi
20 baada ya kukidhi Vigezo vya Kisheria kama vilivyoainishwa katika
Miundo yao ya Utumishi pamoja na kutengewa fedha katika Makisio ya Ikama
na Bajeti ya Mishahara ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2015/2016. Aidha,
Wizara iliwabadilisha kada jumla ya watumishi watatu wa kada tofauti
baada ya kujiendeleza kitaaluma wakiwa kazini na kupata sifa stahiki.
Vilevile, watumishi 29 wamethibitishwa kazini na watumishi 15 wa kada
mbalimbali walithibitishwa katika vyeo vyao vipya baada ya kukidhi vigezo.
188. Mheshimiwa Spika, katika
kuhakikisha kuwa Wizara inawajengea uwezo wa kitaaluma watumishi wake
ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi, Wizara
iliandaa na kutekeleza mpango mdogo wa mafunzo kwa mwaka wa fedha
2015/2016 ambao hadi kufikia mwezi Februari 2016 watumishi wawili (2)
walihudhuria mafunzo ya muda mrefu na watumishi tisa (9) walihudhuria
mafunzo ya muda mfupi. Mpango huu mdogo ni utekelezaji wa mpango wa mafunzo wa Wizara wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018.
USIMAMIZI WA MAPATO NA MATUMIZI
189. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika Mapato na
Matumizi ya Fedha za Umma kwa kuzingatia sheria na kanuni za fedha za
umma. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Wizara imeendelea
kupata Hati Safi ya Ukaguzi wa Hesabu. Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15, Fungu
34 na 97 pamoja na balozi 34 zilizokuwepo kwa wakati huo zimepata Hati
Safi. Naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza watendaji wa Wizara na
kuwahimiza waendelee kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo
mbalimbali ya matumizi ya fedha za Serikali.
CHANGAMOTO ZILIZOJITOKEZA KATIKA UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016
190. Mheshimiwa Spika, Changamoto ambazo Wizara imekabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yake ni kama ifuatavyo:
i. Kasi ndogo ya ubadilishaji wa Sheria za Nchi ili kuendana na matakwa ya Itifaki ya soko la pamoja la Afrika Mashariki;
ii. Kasi
ndogo ya sekta binafsi kutumia fursa za biashara na uwekezaji
zitokanazo na mtangamano wa Afrika Mashariki na masoko ya kimataifa; na
uelewa mdogo wa Watanzania kuhusu masuala ya Mtangamano;
iii. Kasi ndogo ya Watanzania kuchangamkia fursa za ajira zilizopo kwenye taasisi za kikanda na kimataifa;
iv. Kuendelea kuibuka kwa vikwazo vipya visivyo vya kiforodha ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; na
v. Wigo mdogo wa uwakilishi nje. Hadi
hivi sasa, Tanzania ina Balozi 35 na Konseli Kuu 3 duniani. Uwakilishi
huu ni mdogo kuweza kukidhi mahitaji ya nchi hususan katika kipindi hiki
ambacho fursa mbalimbali zinaibuka kila kona ya dunia.
191. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto zilizotajwa hapo juu Wizara yangu imejipanga kutekeleza yafuatayo:
i. Kuendelea
kuzihimiza sekta husika kutoa kipaumbele na kuongeza kasi ya
ubadilishaji wa sheria zilizoainishwa ili kuwawezesha Watanzania
kunufaika ipasavyo na fursa za soko la pamoja;
ii. Kuendelea
kutoa elimu kwa umma kuhusiana na fursa zitokanazo na ushiriki wa nchi
yetu katika Jumuya za kikanda na kimataifa, na kupitia makubaliano na
mikataba mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha Watanzania kuzitumia
ipasavyo;
iii. Kuendelea kuhamasisha Watanzania kujitokeza pindi fursa za ajira zilizopo kwenye taasisi za kikanda na kimataifa zinapotangazwa;
iv. Kuendelea
kuratibu uondoaji wa vikwazo visivyo vya kiforodha nchini ili kuwavutia
wafanyabiashara kutoka ndani ya Jumuiya kununua bidhaa zinazozalishwa
nchini na kutumia bandari zetu kikamilifu; na
v. Wizara itaendelea kuimarisha Balozi zetu na kufungua ofisi za uwakilishi kwenye maeneo yenye maslahi kwa taifa.
SHUKRANI
192. Mheshimiwa Spika, Wizara imefanikiwa kutekeleza
sehemu ya majukumu yaliyotajwa hapo juu kwa ushirikiano na washirika
wa maendeleo kutoka nchi na asasi mbalimbali za kitaifa, kikanda,
kimataifa pamoja na sekta binafsi. Naomba nitumie fursa hii kuwashukuru
washirika wetu wote wa maendeleo ikiwa ni pamoja na Australia, Brazil, Canada, China, Cuba,Denmark, Finland, India, Italia, Ireland, Japan, Korea Kusini, Kuwait, Malaysia, Marekani, Malta, Norway, Oman, Poland, Qatar, Sweden,
Ubelgiji, Ufaransa, Uhispania, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Umoja wa
Falme za Kiarabu, Ureno, Urusi, Uswisi, Uturuki, Umoja wa Ulaya, AfDB, African Capacity Building Facility, FAO, IAEA, ILO, IMF, IOM, Investment Climate Facility for Africa,UNDP, UNEP, UN-HABITAT, UNWTO, UNHCR, UNICEF, UNFPA, UNESCO, UNIDO, WHO, TradeMark East Africa, The Association of European Parliamentarians with Africa, World Bank na WWF kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa Diplomasia ya uchumi.
MALENGO YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017
193. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2016/2017, pamoja na mambo mengine, Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepanga kutekeleza malengo makuu
muhimu kulingana na majukumu yake kama ifuatavyo:-
i. Kuitangaza
nchi yetu kama moja ya nchi duniani zenye mazingira mazuri kwa ajili ya
uwekezaji kutokana na historia yake ya miaka mingi ya amani, umoja,
utulivu na mshikamano wa kitaifa;
ii. Kuongeza uwakilishi wetu nje ya nchi kwa kufungua Balozi mpya, Ofisi za Kikonseli na kuimarisha rasilimali watu na fedha;
iii. Kuendelea
kusimamia, kufuatilia na kuratibu utekelezaji wa mikataba mbalimbali
iliyosainiwa kati ya nchi yetu na nchi nyingine na ile ya mashirika ya
kikanda na kimataifa;
iv. Kukamilisha
mchakato wa kuitambua jumuiya ya watanzania wanaoishi ughaibuni na
kuweka utaratibu utakaowawezesha kuchangia maendeleo ya taifa;
v. Kuratibu
majadiliano kuhusu maeneo ya ushirikiano katika uendelezaji wa
miundombinu ya kiuchumi, kijamii na kuendeleza ushirikiano katika sekta
za uzalishaji;
vi. Kuratibu
utekelezaji wa Mpango Kazi wa miaka kumi wa Umoja wa Fedha katika
kuelekea kwenye eneo la Sarafu Moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
vii. Kuratibu
majadiliano na kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano wa
kiuchumi kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya nyingine za
Kikanda kuhusu kuanzisha Eneo Huru la Kibiashara na Kiuchumi;
viii. Kuratibu, kushiriki na kusimamia majadiliano na utekelezaji wa makubaliano katika maeneo ya siasa, ulinzi na usalama;
ix. Kuratibu, kushiriki na kusimamia majadiliano na utekelezaji wa hatua za Mtangamano wa Afrika Mashariki; na
x. Kutoa Elimu kwa Umma kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki na fursa zinazopatikana katika Jumuiya hiyo.
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017
194. Mheshimiwa Spika, ili kuweza kutekeleza kikamilifu majukumu, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Wizara imepangiwa bajeti ya kiasi cha shilingi 151,396,775,000.00 Kati ya fedha hizo shilingi 143,396,775,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 8,000,000,000.00 ni kwa ajili ya bajeti ya Maendeleo.
195. Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2016/2017, shilingi 133,056,021,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na shilingi 10,340,754,000.00 ni kwa ajili ya Mishahara. Kati ya fedha za Matumizi Mengineyo shilingi 720,160,000.00 ni
kwa ajili ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Tanzania, shilingi
3,154,721,000.00 ni kwa ajili ya fedha za Mishahara na Matumizi
Mengineyo ya Chuo cha Diplomasia na shilingi 686,298,378.00 ni kwa ajili ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.
196. Mheshimiwa Spika, katika
fedha za bajeti ya maendeleo za kiasi cha shillingi 8,000,000,000.00
zilizopangwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017, kiasi cha
shilingi 2,375,250,000.00 zitatumika kufanikisha ujenzi wa jengo la
ofisi ya Wizara ambalo ni sehemu ya Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha
Julius Nyerere; shilingi 1,316,435,000.00 zitatatumika kukamilisha
ukarabati jengo la ghorofa tisa (9), makazi ya Balozi na Mkuu wa Utawala
Ubalozi wa Tanzania Maputo, Msumbiji; shilingi 2,172,880,000.00
zitatumika kukarabati makazi ya Balozi na watumishi yaliyopo Stockholm,
Sweden; shilingi 1,813,871,000 zitatumika kukarabati majengo mawili
yanayomilikiwa na Serikali yaliyopo Khartoum, Sudan na shilingi
321,564,000.00 kwa ajili ya kuboresha mfumo wa mawasiliano kati ya Wizara na Balozi za Tanzania nje.
197. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara kupitia Balozi zake, inatarajia kukusanya kiasi cha shilingi 24,001,150,000.00 kama maduhuli ya Serikali.
HITIMISHO
198. Mheshimiwa Spika, ili
kuweza kutekeleza kikamilifu majukumu yaliyotajwa hapo juu, kwa mwaka
wa fedha 2016/2017, naomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya
Shilingi 151,396,775,000.00. Kati ya fedha hizo Shilingi 143,396,775,000.00. ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi8,000,000,000.00. ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.
199. Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, na Waheshimiwa Wabunge kwa kunisikiliza.
200. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.